Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alipongeza msaada wa chakula unaofika Sudan lakini akasema hautoshi alipotembelea kituo cha mpakani nchini Chad kushuhudia kupitishwa kwa msafara wa misaada ya kibinadamu.
Amina Mohammed, wakati wa ziara yake siku ya Ijumaa kwenye kivuko cha mpaka cha Adre, pia alitoa wito wa kupatikana kwa suluhu katika mapigano nchini Sudan.
Wakati wa mazungumzo ya hivi majuzi huko Geneva, pande zinazozozana zilichukua hatua ndogo kumaliza mapigano lakini ziliahidi kuruhusu misaada ya kibinadamu kupita katika maeneo mawili muhimu ya mpaka.
Ripota wa AFP aliweza kuona msafara wa misaada ya kibinadamu ukivuka mpaka na kuingia jimbo la Darfur nchini Sudan wakati wa ziara ya Mohammed.
Kutimiza ahadi
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilisema katika taarifa siku ya Alhamisi kwamba malori yake yamesafirisha zaidi ya tani 630 - zinazotosha watu karibu 55,000 - kutoka Chad hadi eneo la Darfur.
Mohammed alisema wakati wa ziara yake huko Adre kwamba hii ilikuwa "kiasi kidogo" cha kile kilichohitajika kukabiliana na mateso nchini Sudan.
Alisema Umoja wa Mataifa ulikuwa na uwezo wa kufadhili takriban asilimia 25 hadi 30 ya mahitaji, na kwamba "ahadi zilizotolewa na serikali zinahitaji kutimizwa ili tuweze kuwasaidia watu wanaohitaji duniani.
"Mapigano yalizuka nchini Sudan mwezi Aprili 2023, yakihusisha jeshi la taifa linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan dhidi ya Vikosi vya Kijeshi vya RSF vinavyoongozwa na naibu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Dagalo.
Mashirika ya misaada yanasema mapigano hayo yamezuia misaada ya kibinadamu kuwafikia Wasudan milioni 25 wanaokabiliwa na njaa kali.