Sudan Kusini yawatimua wakuu wa jeshi, polisi na benki kuu

Sudan Kusini yawatimua wakuu wa jeshi, polisi na benki kuu

Tangazo la Rais Salva Kiir halikutoa sababu za wakuu hao kufutwa kazi.
Tangazo la Rais Kiir halikutoa sababu za kufutwa kazi kwa viongoiz hao/  Picha Serikali ya Sudan Kusini X  

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amemfuta kazi Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo, Mkuu wa Polisi na Gavana wa Benki Kuu, kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kupitia Shirika la Utangazaji la Serikali SSBC.

Tangazo la Rais Kiir halikutoa sababu za kufutwa kazi kwa viongozi hao na kuongeza kuwa, Rais Kiir amemteua Paul Nang Majok kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, akichukua nafasi ya Jenerali Santino Wol.

Vyanzo vya usalama vinavyofahamu kinachoendelea katika jeshi hilo vilisema mabadiliko hayo yanaweza kuwa yametokana na hali ya wasiwasi ndani ya safu ya jeshi, na kuongeza kuwa baadhi ya wanajeshi hawajalipwa mishahara kwa takriban mwaka mmoja.

Msemaji wa jeshi Meja Jenerali Lul Ruai Koang hakujibu mara moja alipotafutwa ili kutoa maoni yake.

Usalama wa Taifa

Michael Makuei, Waziri wa Habari na Msemaji wa Serikali, hakujibu mara moja ombi la kutoa maoni juu ya sababu za mabadiliko hayo.

Mwishoni mwa Novemba, jaribio la kumkamata mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi lilisababisha kuzuka kwa milio ya risasi katika mji mkuu, Juba.

Mapema Oktoba, Kiir alikuwa amemfukuza kazi Akol Koor Kuc, ambaye alikuwa ameongoza Huduma ya Usalama wa Kitaifa tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru kutoka kwa Sudan mwaka 2011, na kumteua mshirika wake wa karibu kuchukua nafasi yake.

Katika tetesi za hivi punde, Kiir pia alimuondoa James Alic Garang kama Gavana wa Benki Kuu, na kumrejesha Johnny Ohisa Damian kwenye wadhifa huo baada ya kumfukuza kazi Oktoba 2023.

Alimtaja Abraham Peter Manyuat kama Inspekta Jenerali mpya wa Polisi, akichukua nafasi ya Atem Marol Biar.

Historia ya mabadiliko ya ghafla ya uongozi wa serikali, haswa katika Wizara ya Fedha na Benki Kuu, yamekuwa ya mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, na mnamo 2020 pekee Gavana wa Benki Kuu amebadilishwa mara mbili.

Uchumi wa Sudan Kusini umedorora tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 2013, na kulazimisha takriban robo ya wakazi wake kukimbilia nchi jirani.

Sudan Kusini imekuwa na amani rasmi tangu mkataba wa 2018 uliomaliza mzozo wa miaka mitano uliosababisha mamia ya maelfu ya vifo, lakini ghasia kati ya jamii hasimu huibuka mara kwa mara.

Taifa hilo changa limeahirisha uchaguzi wa kitaifa uliocheleweshwa kwa muda mrefu hadi Disemba 2026, baada ya kubainika kwamba, mifumo ya nchi hiyo, bado haijakuwa tayari kuandaa uchaguzi wa haki na huru.

TRT Afrika