Majadialiano yanahusisha serikali ya Sudan Kusini inayoongozwa na Rais Salva kiir Mayardit na makundi nane ya kisiasa yasiyo na silaha / Picha : Ikulu Kenya

Mchakato wa Upatanishi wa Sudan Kusini nchini umezinduliwa nchini Kenya.

Majadiliano yanahusisha serikali ya Sudan Kusini inayoongozwa na Rais Salva kiir Mayardit na makundi nane yasiyo na silaha ili kuhakikisha changamoto za kisiasa zinafutiliwa mbali.

"Kupitia upatanishi ulioongozwa katika mchakato wa amani uliofanyika Kenya, makubaliano ya amani ya kina yalifikiwa ambayo yalimaliza mzozo mrefu zaidi barani Afrika na kuleta uhuru wa Jamhuri ya Sudan Kusini mnamo 2011," Rais Salva Kiir Mayardit alisema katika mkutano huo uliofanyika jijini Nairobi.

"Nina imani kuwa juhudi hizi sasa zitapata matokeo sawa huku nchi inapojiandaa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu," Rais Salva Kiir ameongezea.

Majadiliano ya upatanishi yanaongozwa na Kenya chini ya wapatanishi wawili wakuu Jenerali Lazarus Sumbeiyo na balozi Mohamed Ali Guyo. Wawili hao walihusika katika kuisaidia Sudan Kusini kufikia makubaliano ya amani mwaka 2018.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema serikali yake ipo tayari kufanya maongezi na makundi mengine nchini / Picha Ikulu Sudan Kusini 

Kwa upande wake, Rais William Ruto wa Kenya amesema Kenya iko tayari kusaidia Sudan Kusini kumaliza mgogoro unaoendelea nchini humo.

"Njia mulioichagua ni nzuri, na kile ambacho mumetimiza hadi sasa chini ya mpango huu ni cha kupendeza. Hapa kuna fursa yenu ya kubuni mustakabali unaostahili maono ya nchi yenu,” Rais William Ruto wa Kenya alisema katika uzinduzi wa maongezi hayo.

Mwaka 2018 serikali ya Salva Kiir na upinzani ukiongozwa na naibu wake wa sasa Riek Machar walitia saini makubaliano ya kuunda serikali ya mpito. Lakini kuna makundi ya upinzani yasiyo na silaha ambayo yalikaa kuwa sehemu ya makubalino hayo.

Mchakato ya maongezi kati ya makundi hayo na serikali yalianza Roma yakiongozwa na Jumuiya ya Sant Egidio, vuguvugu ya ulimwenguni iliyopo Roma.

Ni makundi hayo na serikali ambayo hivi sasa yanafanya mazungumzo yanayoongozwa na Kenya.

Jitihada hiyo imepewa jina la "Mchakato wa Tumaini."

"Kwa sasa, Sudan Kusini inakumbwa na changamoto tena ya kusambaratika ikiwemo changamoto ya kikatiba, inaongozwa na katiba ya mpito na matamshi ya rais ambayo huzingatiwa kama sheria. Hamu ya watu wa Sudan Kusini ni kujipatia katiba ya kudumu ambayo haionekani kufikiwa," Pagan Amum mwakilishi wa makundi hayo yasiyo na silaha alisema katika mkutano wa Nairobi.

"Nchi pia ina shida ya serikali ambayo haiwezi kuleta amani na huduma kwa wananchi wake na kuwarudishia watu nguvu ya kufanya uchaguzi wa wazi," aliendelea kusema.

Pagan Amum Pagan Amum mwakilishi wa makundi yasiyo na silaha / Picha: Ikulu Kenya 

Riek Machar ambaye aliongoza upinzani katika kutia saini makubalino na serikali 2018 sasa amekuwa sehemu ya seriklai katika maongezi haya. Hata hivyo, ameteuwa mawaziri wake watatu ambao wanamuwakilisha.

Baada ya kupata uhuru mwaka 2011, Sudan Kusini iliingia katika vita vya ndani Disemba 2013. Hii ilifuatia mvutano kati ya rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake wakati huo Riek Machar. Vita hivi vilifungua wimbi la matatizo ya kibinadamu, hivyo kusababisha zaidi ya watu milioni mbili kuhama makazi yao huku wakitoroka vita.

"Makubaliano yote na mipango ya uongozi wa muda haijafikisha Sudan Kusini katika amani," Amum amesisitiza.

"Serikali sasa haina uwezo wa kulipa wafanyakazi wake au kufanya maendeleo yoyote muhimu au hata kuwezesha balozi zake kufanya kazi. Hii imepelekea mabalozi wengine kuondolewa kwa makazi yao kama ilivyofanyika Roma siku mbili zilizopita," Amum amesema.

Makundi haya yasiyo na silaha yamesema yanataka serikali kujitolea kumaliza vita zilivyoleta mgawanyiko katika kijamii na kuwawezesha wananchi wa Sudan Kusini kurejea nyumbani kwa amani na kuishi bila uwoga.

Wapatanishi wanasema kutimiza haya kutahitaji pande zote mbili kufanya majadiliano kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wake.

"Kuendelea na maongezi na makubaliano ya masuala nyeti itawezekana ikiwa washikadau watafuata mpango na utaratibu tuliokubaliana," Mpatanishi Mkuu Lazarus Sumbeiyow amesema .

"Wahusika wajadiliane kwa nia njema na kuzingatia umuhimu wa amani. Upatanishi huu unatoa fusra ya kunyamazisha bunduki na kuwapa watu wa Sudan Kusini amani. Inabidi tujifunze kutokana na somo lililopita lililo wazi kwamba utekelezaji wa makubaliano kuhusu Sudan Kusini umesalia kuwa changamoto," Sumeiyow ameongezea.

Uzinduzi wa mazungumzo haya ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi hayo nane yasiyo na silaha ulihudhuriwa na marais Lazarus Chakwera wa Malawi, Hakainde Hichilema wa Zambia, Nangolo Mbumba wa Namibia na Faustin-Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

TRT Afrika