Huku Jamhuri ya Sudan Kusini ikiadhimisha miaka 12 ya uhuru wa nchi hiyo, rais Salva Kiir amewataka raia wa Sudan Kusini kukumbatia moyo wa amani na maridhiano.
"Tunahitaji utulivu ili kuruhusu watu wetu kurejea nyumbani kwa hiari kutoka kwenye kambi za wakimbizi ili kuruhusu kufanya maelewano na serikali iweze kufanya uchaguzi wa kuaminika," Rais Salva Kiir aliambia wananchi katika taarifa.
"Kupata amani na utulivu ndio njia pekee itakayotuwezesha kujiondoa kwenye mzunguko wa serikali za mpito na vurugu na kuleta amani ya kudumu."
Sudan Kusini iliingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya 2013 na 2018 baada ya mvutano wa uongozi kati ya Rais Salva Kiir na makamu wake wa wakati huo Riek Machar.
Rais Kiir ameita vita hivi "vita visivyo na maana".
Bado utulivu haujarejea kamili nchini humo.
Shirika la Umoja wa mataifa la kutetea wakimbizi linaonyesha kuwa watu milioni 2 wamehama ndani ya Sudan Kusini, kutokana na migogoro, ukosefu wa usalama na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mgogoro wa Sudan Kusini bado unaangaliwa kama mkubwa zaidi barani Afrika, huku zaidi ya wakimbizi milioni 2.3 wa Sudan Kusini wakihifadhiwa kwa ukarimu katika nchi jirani, haswa Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda.
Makubaliano ya amani kati ya pande hizi mbili na makundi mengine ambayo yalihusika pia katika vita hivyo yalitiwa saini mwaka 2018, kwa nia ya kuunda serikali ya mpito.
Zaidi ya wakimbizi 500,000 wa Sudan Kusini wanaripotiwa na Umoja wa mataifa wamerejea nchini tangu kusainiwa kwa mkataba huu wa amani.
Chini ya makubaliano haya Riek Machar ameteuliwa kama makamu wa rais.
Makubaliano haya yanahitaji Sudan Kusini kufanya uchaguzi mkuu kwa ajili ya kupitisha uongozi kwa serikali thabiti.