Rais Salva Kiir amesema kupata uhuru wa Sudan Kusini ilikuwa ni safari ngumu iliyokuwa na gharama kubwa/ Picha Wengine 

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Miaka 13 iliyopita, tarehe 9 Julai 2011, Sudan Kusini ilipata uhuru wake. Sudan Kusini, ni nchi changa kabisa barani Afrika, ambayo ilikuwa sehemu ya Sudan.

Nchi hiyo ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inakadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 10.

Rais wa nchi hiyo Salva Kiir amesema kuwa kupata uhuru wa Sudan Kusini ilikuwa ni safari ngumu iliyokuwa na gharama kubwa. Akielezea kuwa mapambano ya uhuru wa nchi hiyo yalianza mapema tangu mwaka 1947.

Hata hivyo, licha ya kuadhimisha muongo mmoja wa uhuru wake, wananchi wa Sudan Kusini hawajaonja utamu wa uhuru kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoibuka miaka miwili tu baada ya kupata uhuru. Mapigano yalihusisha vikundi vinavyomuunga mkono Rais Salva Kiir na Makamu wake wa wakati huo Riek Machar.

Zaidi ya watu milioni 4.4 walilazimika kuhama makazi yao, huku wengine zaidi ya milioni 2 wakikimbilia nchi jirani ikiwemo Sudan, ambapo hivi sasa wamelazimika kurudi kutokana na vita vilivyoibuka nchini Sudan tangu Aprili 2023.

Vita nchini Sudan Kusini ilipeleka wakimbizi zaidi ya milioni 4.4  / Picha : Norwegian Refugee Council

Makubaliano ya amani ya 2015 yaliyoporomoka 2016

Maafikiano mapya yalifikiwa 2018 kwa Rais Kiir kuunda serikali ya muda na Riek Machar.

Uongozi huu wa muda ulipangwa kumalizika Februari 2023, lakini Agosti 4, 2022, wahusika katika mkataba huo walikubaliana kuurefusha kwa miezi mengine 24.

Nchi hiyo sasa inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu kwa mara ya kwanza Disemba 22, 2024.

Ingawa tarehe rasmi ya uchaguzi tayari imepangwa, lakini bado kuna masuala kadhaa ambayo hayajatimizwa kama kuundwa kwa katiba, kufanya sensa ya kitaifa, kuunda mifumo ya sheria na jeshi la pamoja. Jamii ya kimataifa imejaribu kuishawishi Sudan Kusini kuahirisha uchaguzi huo, lakini Rais Kiir amesisistiza kuwa ni muhimu uchaguzi huo kufanyika.

Mvutano kati ya Rais Salva Kiir na makamu wake Riek Machar / Picha: Wengine

Utajiri wa Sudan Kusini

Nchi hiyo, ina utajiri mkubwa ambao ni pamoja na ardhi ya kilimo, maji ya Mto Nile, mali asili kama mafuta, chuma, shaba, zinki, tungsten, fedha na dhahabu. Rasilimali hizi zote hazijatumika ipasavyo kutokana na ukosefu wa hali ya usalama.

Iwapo hali ya utulivu na uongozi bora utapatikana, wataalamu wanasema kuwa Sudan Kusini ina uwezo wa kujiboresha kutokana na mapato ya ndani ya mafuta.

Taifa hilo changa linakadiriwa kuwa na takriban mapipa bilioni 3.5 ya mafuta na kuzalisha wastani wa takriban mapipa 149,000 kwa siku, hii ni kulinganna na takwimu za mwaka wa 2023.

Na ina uwezo wa kuongeza uzalishaji wa hadi takriban 160,500 ifikapo 2027.

Inapoadhimisha tena siku yake ya kupata uhuru, wataalamu wanasema uongozi utakaochaguliwa Disemba 2024, utakuwa na jukumu la kutimiza ndoto za wananchi wa taifa hilo ili waweze kufurahia matunda ya uhuru ambayo hawajawahi kuyaonja.

TRT Afrika