Uchumi wa Sudan Kusini kwa kiasi kikubwa unategemea mafuta yanatouzwa nchi jirani ya Sudan / Picha: Reuters

Tukio la kupasuka bomba la mafuta nchini Sudan Kusini hivi karibuni kumesababisha changamoto mpya katika uchumi wa nchi hiyo, huku vikosi vya usalama nchini humo vikilazimika kuishi bila mishahara.

Hatua hiyo imewafanya baadhi ya askari na watumishi wengine wa umma kugeukia shughuli nyingine ili waweze kujikimu kimaisha.

Kwa kiasi kikubwa, uchumi wa Sudan Kusini unategemea mafuta, bidhaa inayouza nje kupitia nchi jirani ya Sudan.

Lakini machafuko yanayoshuhudiwa Sudan na kupasuka kwa bomba kubwa la mafuta mwezi Februari mwaka huu, kumefanya hali ya maisha kuwa mbaya zaidi nchini humo.

Kwa sasa, taifa hilo linashuhudia maandamano katika mji mkuu wake huku ukosefu wa malipo kwa watumishi wa umma ukitarajiwa.

Hatua hiyo imewalazimu baadhi ya watu kutafuta shughuli zingine za kiuchumi.

Katika mji mkuu, Juba, naibu mwalimu mkuu wa shule, Maburuk Kuyu Surur, alisema amekuwa akifundisha kwa miaka 36 na hajawahi kuona ucheleweshwaji wa mshahara kama huu.

Hilo lilianza miaka ya nyuma kabla ya Sudan Kusini kujinyakulia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011.

Ofisi tupu

Surur alisema yeye na walimu wengine wamekuwa wakikusanya pesa kidogo kutoka kwa familia za wanafunzi ili kusaidia kujikimu, ingawa shule ni bure.

"Tunateseka," mzee wa miaka 60 alisema.

Serikali ya Rais Salva Kiir, ambaye ameiongoza Sudan Kusini tangu uhuru inakabiliwa na shinikizo la kimataifa la kuchelewesha uchaguzi nchini humo, huku nchi hiyo ikiwa imeathirika na mizozo ya kiuchumi.

Wizara ya fedha imekuwa na mawaziri sita tangu 2020, na waliofutwa kazi hivi karibuni mnamo Julai.

Katika wiki za hivi karibuni, wizara nyingi za serikali na afisi zingine huko Juba zimekuwa tupu wakati wa muda wa kazi. Wafanyakazi waliosalia wameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba wafanyakazi wenzao waliondoka baada ya kuchoka kufanya kazi bila malipo tangu Oktoba.

Mfanyakazi mmoja wa serikali alisema mshahara wake - ulipowadia - ulikuwa sawa na dola 8 za Kimarekani kwa. Tangu wakati huo amepata kazi katika mkahawa mmoja na anatengeneza takriban Dola 20. Alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuhofia kudhulumiwa. "Bei zinaendelea kupanda kila siku," alisema.

Mfuko wa kilo 50 wa unga wa mahindi sasa unagharimu hadi mara tano ya bei mwaka mmoja uliopita.

Mfumuko wa bei nchini Sudan Kusini ni asilimia 35 kutoka mwaka mmoja uliopita, kulingana na Benki ya Dunia. Wakati huo huo, sarafu ya ndani imeshuka dhidi ya dola ya Marekani kwenye soko la fedha na katika kiwango rasmi.

Kuzuia rushwa

Licha ya kuwa thuluthi moja ya mafuta ya Sudan Kusini bado yanasafirishwa kwa mauzo ya nje kupitia bomba lingine, Rais wa nchi hiyo ameeleza waziwazi kuchoshwa na usimamizi mbovu kwani serikali lazima itegemee zaidi mapato yasiyo ya mafuta kama vile ushuru katika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Mapato hayo yanapaswa kutosha kufidia mishahara lakini pesa hazifikii akaunti za serikali, Kiir alisema Julai.

"Tuna miezi tisa watu hawajapata mishahara yao, na tuna pesa," alisisitiza baada ya kumuapisha waziri wa fedha . Kiir alimuagiza Waziri huyo kuanzisha akaunti moja ya mapato yote na kukabiliana na vitendo vya rushwa katika ukusanyaji wa mapato.

Serikali haikuwa imeweka mkazo zaidi katika hili hapo awali wakati mafuta mengi yalikuwa yakitoka, alisema Boboya James, afisa mkuu mtendaji wa Taasisi ya Sera ya Kijamii na Utafiti yenye makao yake makuu mjini Juba.

Kucheleweshwa Uchaguzi

Alisema kudorora kwa fedha za umma kunatokana na sera mbovu na ufisadi ambao umeliibia taifa changa fedha za maendeleo.

Hivi karibuni, benki ya Maendeleo ya Afrika na serikali ya Sudan Kusini hivi karibuni zilitia saini mkataba wa dola milioni 46.2 kusaidia uzalishaji wa kilimo hadi Desemba 2030.

Vurugu kati ya jamii zinaendelea hata baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka iliyopita.

Uchaguzi huo ambao ulikuwa umepangwa kufanyika mwaka jana umeahirishwa hadi Desemba, lakini Umoja wa Mataifa unasema kazi inayohitajika kuutekeleza haijakamilika.

Uhamaji na umaskini katika nchi isiyo na bandari umeenea. Umoja wa Mataifa umesema asilimia 75 ya watu wanategemea misaada ya kibinadamu.

Sudan Kusini inatarajia kubadilisha mapato yake kwa utalii na kilimo cha matunda na mboga mboga, miongoni mwa mawazo mengine.

TRT Afrika