Vikosi vya usalama nchini Somalia vimefanikiwa kuwaua magaidi 304 wenye mahusiano na kikundi cha al-Qaeda ndani ya miezi miwili, maofisa wa nchi wamesema siku ya Jumanne.
Mauaji hayo yalifanyika kupitia operesheni maalumu zilizofanywa na idara ya kijasusi ya Somalia (NISA) na washirika wengine katika maeneo ya kusini na kati ya nchi hiyo.
Kulingana na NISA, operesheni hizo zilifanyika katika eneo la Yaaqle na Shabelle, na kuwauwa magaidi wapatao 27 na kujeruhi wengine zaidi ya 30.
“Operesheni hii inalenga kuwaondoa magaidi hasa mabaki ya wafuasi wa Khawarij ambao wanaendelea kunyanyasa watu wa Somalia,” ilisema idara hiyo kupitia taarifa yake.
Kukombolewa kwa vijiji
Kulingana na NISA, taarifa zilikuwa zinatolewa kwa raia kuhusu kusogea mbali na maeneo yanapofanyika operesheni hizo.
Zaidi ya magaidi 100 wa kikundi cha al-Shabaab waliuwawa na kujeruhiwa katika operesheni kama hizo zilizofanyika Bida Isse na Geriile, kulingana Mkuu wa Jeshi la Somalia.
Ukosefu wa amani
Nchi ya Somalia, ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa vitani kwa muda mrefu sasa.
Nchi hiyo, imekuwa ikipambana na kikundi cha al-Shabaab toka mwaka 2007.
Kikundi hicho kimeongeza kasi ya mashambulizi, hususani baada ya Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kutangaza vita dhidi yake.