Mkuu wa Jeshi la Somalia Meja jenerali Odawaa Yusuf Rageh amefutwa kazi.
Mkutano wa baraza la mawaziri uliofanyika siku ya Jumatatu, na kuongozwa na waziri mkuu Hamza Abdi Barre, uliamua kumsimamisha kazi Rageh huku Somalia ikizidisha mapambano yake dhidi ya kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab.
Baraza la mawaziri pia liliidhinisha uteuzi wa Brigedia-Jenerali Ibrahim Sheikh Muhiyadin Addow kama Mkuu mpya wa Jeshi la Kitaifa la Somalia, taarifa ya ofisi ya waziri mkuu ilisema.
"Baraza la Mawaziri limeidhinisha pendekezo la Wizara ya Ulinzi la kuteuliwa kwa Kamanda wa Jeshi la Taifa la Somalia na kumteua Brigedia Jenerali Ibrahim Sheikh Muhyadin Addow," taarifa hiyo ilisema.
Mkuu huyo mpya wa jeshi hapo awali aliwahi kuwa kamanda wa walinzi wa rais, na inasemekana alisomea masuala ya kijeshi nchini Italia.
Afisa huyo wa zamani, Rageh, aliteuliwa kuwa mkuu wa jeshi mnamo Agosti 2020 na rais wa zamani Mohamed Abdullahi Farmajo.
Kufutwa kwake kunakuja huku kukiwa na mvutano wa kisiasa katika eneo la Hiran katika jimbo la Hirshabele, kitovu cha jeshi linalopambana dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab.
Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya kiongozi wa Hirshabele, Ali Gudlawe Hussein, kumfuta kazi Ali Jeyte Osman, gavana wa utawala wa eneo la Hiran, ambaye alionekana kuwa uso wa vita dhidi ya kundi la kigaidi katika jimbo hilo.
Hata hivyo, Osman alipinga kufutwa kazi na akatangaza kwamba hatalitambua tena jimbo hilo. Alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Beldwayne, mji mkuu wa eneo la Hiran, Jumapili.