Somalia yaapa kulinda ardhi yake kufuatia mkataba wa Bandari wa Ethiopia na Somaliland

Somalia yaapa kulinda ardhi yake kufuatia mkataba wa Bandari wa Ethiopia na Somaliland

Somalia pia imemuita nchini balozi wake wa Ethiopia kwa majadiliano juu ya mkataba huo wa Bandari na Somaliland.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akilihutubia bunge la Somalia. Picha: Ikulu Somalia

Viongozi wa Somalia akiwemo rais Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre wameapa kuwa Somalia italinda eneo lake kwa "njia zote za kisheria zinazowezekana" kufuatia makubaliano ya Jumatatu ambayo yanaipa Ethiopia isiyo na pwani ufikiaji uliotafutwa kwa muda mrefu wa Bahari Nyekundu.

Serikali ya Somalia imesema kuwa mkataba uliosainiwa na eneo lake lililojitenga la Somaliland na Ethiopia wa kuiruhusu kutumia bandari ya Bahari Nyekundu ya Berbera sio halali, na kuongeza kuwa ilihatarisha utulivu wa eneo hilo.

Makubaliano ya Jumatatu, yaliyotiwa saini mjini Addis Ababa kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais wa Somaliland Muse Bihi Abdi, yataifungulia Ethiopia njia kuanzisha shughuli za kibiashara za baharini na kuipa ufikiaji wa kituo cha kijeshi kilichokodishwa kwenye Bahari ya Shamu, mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Abiy Redwan Hussien alisema.

"Hakuna mtu mwenye idhini au mamlaka ya kugawa sehemu yoyote ya Somalia. Babu zetu, baba, mama, bibi walikataa, nasi pia tunakataa," rais Hassan Sheikh Mohamud alisema.

"Kama Serikali, tumelaani na kukataa ukiukaji haramu wa Ethiopia dhidi ya uhuru wetu wa kitaifa na uadilifu wa eneo. Hakuna hata inchi moja ya Somalia inayoweza kutolewa na mtu yeyote. Somalia ni ya watu wa Somalia."

Somalia pia imemuita nchini balozi wake wa Ethiopia kwa majadiliano juu ya mkataba huo wa Bandari na Somaliland huku ikitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusimama kando yake juu ya "shambulio la wazi" dhidi ya uhuru wake.

Mkataba huo pia ulijumuisha kuitambua Somaliland kama taifa huru kwa wakati unaofaa.

Serikali ya Somalia pia ilisema inaomba Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Kiarabu na jumuiya ya kikanda ya Afrika Mashariki na IGAD miongoni mwa wengine "kusimama na haki ya Somalia kutetea uhuru wake na kulazimisha Ethiopia kufuata sheria za kimataifa."

"Nataka kukuhakikishia kuwa tumejitolea kutetea nchi, hatutaruhusu hata inchi ya ardhi, bahari na anga kukiukwa," alisema Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza.

Somaliland haijapata kutambuliwa kimataifa, licha ya kujitangaza huru kutoka Somalia mwaka 1991. Somalia inasema Somaliland ni sehemu ya eneo lake.

TRT Afrika na mashirika ya habari