Bunge la Somalia limepitisha muswada wa marekebisho ya uchaguzi, na kuelekea kwenye upigaji kura kwa wote baada ya miongo kadhaa ya mfumo wa upigaji kura unaozingatia koo.
Sheria inayoruhusu kura ya mtu binafsi kupiga kura yake moja kwa moja unachukua sasa nafasi ya mfumo tata wa upigaji kura usio wa moja kwa moja uliopo hivi sasa. Uamuzi huu uliungwa mkono na wabunge 169 wakipiga kura ya ndiyo huku wawili wakipinga na mjumbe mmoja kutopiga kura.
Somalia imekuwa na mfumo wa uchaguzi usio wa moja kwa moja, ambapo wajumbe wa koo ndio wanaochagua wabunge wa kitaifa, ambao humchagua rais.
Chini ya mfumo mpya, rais atachaguliwa moja kwa moja.
Uchaguzi ujao wa urais umepangwa kufanyika 2026.
Marekebisho hayo pia yameunda mfumo wa vyama vingi vya siasa hata hivyo, vyama vitakavyoruhusiwa ni vitatu tu.
Licha ya upinzani kutoka majimbo ya Puntland na Juba, na marais wa zamani, Rais Hassan Sheikh Mohamud, aliyechaguliwa na wabunge mnamo 2022, alitangaza mwishoni mwa Oktoba kwamba vyama vya kisiasa vilikubaliana juu ya mfumo wa upigaji kura kwa wote.