Waziri alielezea kusikitishwa na namna ushawishi potofu unafanyika kupitia vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii  / Picha: Reuters

Waziri wa mawasiliano na teknolojia nchini Somalia amesema kuwa serikali inanuia kufunga mitandao ya Tik Tok na Telegram kama njia moja ya kuzuia kudorora kwa maadili ya watoto nchini humo.

''Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia inajitahidi kulinda tabia ya kimaadili ya jamii ya Wasomali wakati wa kutumia zana za mawasiliano na mtandao ambazo zimeathiri mfumo wa maisha na kuongeza mazoea mabaya,'' Waziri huyo alisema katika taarifa.

Waziri Jama Hassan Khalif ameongoza kongamano Jumapili la kujadili usalama wa mawasiliano, kulinda usalama wa mtandao na mitandao ya kijamii, ambalo limehudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara hiyo Abdiaziz Duwane Isaq, Maafisa kutoka Shirika la Taifa la Mawasiliano na Wakuu wa makampuni ya mawasiliano nchini.

Waziri alielezea kusikitishwa na namna ushawishi potofu unafanyika kupitia vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii ambazo alisema zinaeneza tamaduni zisizokubalika nchini humo.

''Kutekeleza jukumu hili ni wajibu wa Shirika la Taifa la Mawasiliano na makampuni yanayofanya kazi katika masuala yanayohusiana na TEHAMA.'' Taarifa iliendelea kusema.

Taarifa hiyo pia imeelezea kuwa mkutano ulikubaliana kufunga kampuni ya kucheza kamari ya 1XBET ambayo imelaumiwa kuvunja maadili ya kidini.

Somalia ni taifa lenye idadi kubwa zaidi ya waumini wa dini ya kiislamu na hutazamiwa kufuata maadili ya kidini pamoja na kimila.

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la vijana wanaotuma video nchini Somalia wakishiriki densi au kuonyesha mavazi, jambo ambalo linakemewa katika jamii hiyo hasa kuhusu watoto wa kike.

''Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia FGS imezindua kampeni ya uhamasishaji kwa umma ili kuonya umma kuhusu hatari za mawasiliano na Mtandao, ambayo hurahisisha usambazaji wa habari za upotoshaji na habari zinazodhuru watu wasio na hatia au uchochezi kwa umma.'' Taarifa iliongezea.

TRT Afrika