Tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka nchini Somalia katika miaka ya 1980, takriban watu milioni mbili, sawa na asilimia 10 ya idadi ya watu, wamekimbia nchi hiyo. Picha: Kwa hisani

Wakati hadithi kuu huko Ulaya na Marekani inahusu 'wimbi kubwa' la wahamiaji 'kufurika' katika pwani zao, lakini kuna upande mwingine wa hadithi hii.

Wengi wa wahamiaji hawafiki mahali wanakotarajia au wanafukuzwa wanapofika huko. Wengine huamua kurudi katika nchi zao.

Tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka nchini Somalia katika miaka ya 1980, takriban watu milioni mbili, sawa na asilimia 10 ya idadi ya watu, wamekimbia nchi hiyo.

Wasomali ni miongoni mwa jamii zilizotawanyika zaidi duniani. Wengi wao wamehamia nchi za Ghuba.

Mara nyingi wanawekwa katika vituo vya uhamisho kabla ya kufukuzwa. Mara nyingi hulalamika juu ya muamala mbaya.

Kutengeneza mkate maalum

Baba wa watoto wanne, Abdikadar Abdirahman Hussein, alirudishwa kutoka Saudi Arabia mwaka 2021 baada ya kuishi huko kwa miaka mingi. Aliporudi Mogadishu, alipambana kujenga upya maisha yake.

Kisha akaibuka na wazo la kipekee. Atawaletea Wasomali chakula cha Saudi Arabia.

Familia yake iliweka dola 500 kumsaidia kuanzisha biashara, mgahawa wa haraka uitwao “Boufiyah Jeddah”. Alikuwa anatumia ustadi wa upishi alioupata nchini Saudi Arabia kutengeneza chakula cha Kiarabu, ikiwa ni pamoja na shawarma, mkate maalum uitwao khubus, na nyama na mchele iliopikwa kwa taratibu inayoitwa “mandi”.

Kibanda chake katika eneo la Hawlwadag la Mogadishu, mara kwa mara kimejaa watu wanaotaka kujaribu aina hii mpya ya chakula. Pia ni maarufu kati ya Wasomali waliotolewa nchini Ghuba ambao wanakumbuka vyakula walivyokuwa wakila huko.

Vinywaji vinavyopendwa zaidi ni juisi iliotengenezwa na matunda freshi na miksheki iliyotengenezwa na embe, ndizi, na tikiti maji yal, na kupambwa na zabibu na njugu iliosagwa.

"Furaha nyumbani

"Nilianza kuuza vyakula rahisi kwa dola 0.50," anasema Bwana Hussein. "Biashara yangu ilikua haraka na sasa ninaajiri vijana sita, wote waliofukuzwa kama mimi," aliiambia TRT Afrika.

Anasema anapata kati ya dola $20 na dola $30 kwa siku, ambayo inatosha kuihudumia familia yake. Wafanyakazi wake wanapata dola $10 kwa siku, na mapato yoyote ziada yanaekezwa katika biashara.

Mtu wa kwanza aliyeajiriwa na Bwana Hussein alikuwa Adde Abdirashid Mohamed aliyetoka Somalia kwenda Saudi Arabia mwaka 2017 kutokana na vurugu na kutokuwa na usalama mara kwa mara. Alirudishwa mwaka 2022.

"Nilikuwa nikinunua chakula kutoka kwenye mkahawa kwa sababu napenda vyakula vya Saudi Arabia," anasema. "Niliona fursa na kumwambia Bwana Hussein najua jinsi ya kupika chakula cha Kiarabu. Alinipa kazi, na shukrani kwake maisha yangu yamebadilika. Nafurahi kuwa nyumbani sasa ninapopata pesa."

'Chakula kitamu'

Mfanyakazi mwingine ni Ahmed Aweys Mohamud. Haikuwa rahisi kwake aliporudishwa kwa nguvu nchini Somalia kwa sababu alihama kwenda Ghuba akiwa mdogo sana na hakujua mengi kuhusu utamaduni wa Kisomali.

"Watu wa Mogadishu walikuwa wanacheka kwa sababu nilikuwa nazungumza Kisomali kisichokuwa fasihi," anasema huku akiangalia chakula kinachoonekana kitamu kwenye sufuria kubwa. "Kisha nikapata kazi katika mkahawa “Boufiyah Jeddah”. Tunaelewana na wamekuwa kama ndugu zangu."

Mtu mwingine aliyefukuzwa na kufanya maendeleo nyumbani nchini Somalia ni Omar Mohamed Osman.

Alipelekwa nchini Marekani mwaka 2021 baada ya kukimbia Somalia mwaka 2012 kutokana na vitisho vya kundi la Al Shabaab. Kwanza alihamia Afrika Kusini na kwenda Marekani mwaka 2017, ambapo baada ya miaka kadhaa, madai yake ya kutaka hifadhi yalikataliwa.

Alipambana sana aliporudi Somalia lakini hatimaye akafungua duka dogo la vyakula kwenye eneo la Waberi huko Mogadishu.

Anasema ana furaha aliponea mwaka wa kwanza uliyokuwa mgumu baada ya kufukuzwa kwake. Omar mwenye umri wa miaka 40 sasa ana mtoto na anapata kipato cha kutosha kuwasaidia familia yake.

Madai ya hifadhi yakikataliwa

Bwana Osman anasema kati ya wanaume 87 waliotolewa naye Marekani, baadhi wamejiunga na jeshi la Somalia. Anasema wengine kadhaa walikufa baada ya kushindwa kujipatia riziki nyumbani huku wengine wakiondoka tena Somalia.

Kijana wa Kisomali, Mohammed (si jina lake halisi), aliyerudishwa Mogadishu baada ya madai yake ya hifadhi kukataliwa nchini Uingereza alidhani maisha yake yamekwisha aliporudi nyumbani.

Kwanza hakuweza kupata mahali pa kukaa au chakula cha kutosha. Polepole, alianza kujenga upya maisha yake.

Kwanza, alijitolea kama kocha wa mpira wa miguu, huku akilipwa hadi dola $1 kwa siku. Kisha akapata kazi ya kibarua cha ujenzi, pamoja na stadi aliyojifunza Uingereza, kama vile kupiga plasta, ilikuwa inahitajiwa sana. Baadaye, alipewa kazi ya kudumu na kampuni ya ujenzi na sasa ameanzisha familia.

Kufundisha wengine

Wanawake waliorudishwa makwao pia wanachangia katika maendeleo ya jamii yao. Baadhi wameubadilisha sekta ya urembo nchini Somalia kwa kuleta mambo mpya, kama vile mitindo tofauti ya kusuka nywele na upodoaji kwa ajili ya harusi.

Kwa kuwa saluni za urembo, kawaida ni za wanawake na zina wafanyakazi wa kike pekee, waliorudishwa wanajisikia salama kufanya kazi katika mazingira kama hayo. Wengine wanaorejea wanapamba kwenye maharusi kwa mitindo waliyoona na kujifunza wakiwa nje ya nchi.

Bila shaka, waliorudishwa wanakabiliana na changamoto nyingi za kuishi, hasa wale wasio na familia au wasiokuwa na watu wa kuwasadia kujianzisha tena nchini Somalia. Wale wanaorudishwa kwa makosa ya jinai, hasa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, wanapuuzwa na baadhi ya wanajamii wao.

Waliorudishwa wanasema kuwa kufukuzwa Somalia kamwe si rahisi na maisha ni magumu mara nyingi wanapofika. Lakini baadhi ya watu wenye ujasiri na ujasirimali wanachangia kuleta umahiri mpya nchini mwao, kufundisha wengine, na kuleta ajira.

Mwandishi, Naima Said Salah, ni mwandishi wa habari Mogadishu, anayefuatilia habari na makala za kina nchini Somalia.

TRT Afrika