Simba amemuua mtaalamu wa teknolojia ya mifugo anayefanya kazi katika Chuo Kikuu kimoja bora nchini Nigeria.
Olabode Olawuyi alikuwa akimtunza mnyama huyo kwa takriban miaka tisa katika bustani ya wanyama ya Chuo Kikuu cha Obafemi Awolowo katika mji wa kusini wa Ile-Ife kabla ya tukio hilo siku ya Jumatatu.
Olawuyi alikatwakatwa na simba huyo mkubwa wakati wa kumlisha na juhudi za wenzake kumuokoa hazikufaulu, msemaji wa chuo hicho, Abiodun Olarewaju alisema katika taarifa.
"Wasimamizi, wafanyakazi, wanafunzi, na chuo kizima Kikuu cha Obafemi Awolowo, Ile-Ife, Jimbo la Osun, wametupwa katika maombolezo kufuatia kifo cha Olabode Olawuyi,'' iliongeza taarifa hiyo.
Simba huyo hatimaye aliuawa, ''kwa njia ya kibinadamu'' kufuatia kifo cha mfanyakazi huyo ''ili kupunguza hofu.''
Ilikuwa wazi mara moja kwa nini simba alimshambulia mlinzi wa bustani. Maafisa wa Chuo Kikuu walisema uchunguzi umeamriwa.
Marehemu alikuwa akisimamia bustani ya wanyama ya Chuo Kikuu kwa zaidi ya muongo mmoja na kumtunza simba huyo tangu alipozaliwa kwenye chuo hicho, mamlaka ilisema.