UNESCO siku ya Alhamisi imeongeza katika orodha yake ya urithi wa utamaduni wa dunia gwaride la Kinigeria ambalo inahusisha wapanda farasi wanaosherehekea sikukuu mbili takatifu zaidi za Waislamu.
Sherehe hizo zinazojulikana kama Durbar - pia huandaliwa katika eneo la kaskazini lenye idadi kubwa ya Waislamu.
Kuanzia karne ya 15, msafara huo uhusisha mtawala mashuhuri wa dini na wapanda farasi 10,000 wakiandamana na wanamuziki katika mitaa ya Kano, jiji kubwa zaidi kaskazini mwa Nigeria.
Tamasha hilo hufanyika mara mbili kwa mwaka katika sikukuu za Eid al-Fitr na Eid al-Adha zinazoadhimishwa duniani kote katika miezi ya 10 na 12 ya kalenda ya Kiislamu, ambayo inafuata awamu za mwezi.
Sherehe zina asili yake Kano, jiji la pili kwa ukubwa nchini Nigeŕia lenye watu milioni nne, makazi ya mmoja wa viongozi wakuu wa kidini katika nchi hiyo.
"Durbar ni tamasha la rangi, heshima, fahari na maelewano," alisema Hajo Sani, ambaye anaiwakilisha Nigeria katika Shirika la Kitamaduni cha Umoja wa Mataifa, katika kikao cha 19 cha Kamati ya Kiserikali ya Kulinda Turathi za Utamaduni zisizogusika uliofanyika katika mji mkuu wa Paraguay Asuncion.
"Ni tamasha kubwa la kitamaduni na kijamii ambalo linaleta pamoja makabila mengi, ikiwa ni pamoja na Wahausa, Wafulani, Waarabu, Wanupe, Wayoruba na Watuareg, hivyo kuwaunganisha katika jumuiya moja," aliongeza.
Akisindikizwa na kikosi cha maafisa wa ikulu, maafisa na walinzi, emir aliyevalia mavazi ya kifahari ndiye mtu mkuu katika kila maandamano.
Kwa nini Durbar ilipigwa marufuku mwezi Juni?
Katika sherehe hizi kiongozi na wasaidizi wake hupita katika vitongoji vya Kano, wakati wenyeji wakitoa heshima zao na kumuonyesha msaada, kulingana na tovuti ya UNESCO.
Tangu jadi Amiri wa Kano ndiye mtawala wa pili muhimu wa Kiislamu nchini baada ya Sultani wa Sokoto, kiongozi mkuu wa kidini kaskazini mwa Nigeria.
Watawala wengi wa jadi wa Nigeria hawana mamlaka ya kikatiba lakini ni walinzi muhimu wa kitamaduni, wakiwa na ushawishi mkubwa katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Polisi wa Kano walipiga marufuku Durbar ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika Juni mwaka huu kutokana na masuala ya usalama, baada ya mvutano kuzuka kati ya machifu wawili wa kimila waliokuwa wakigombea cheo cha kihistoria cha emir huyo.
"Sekta ya kutengeneza ajira"
Durbar inajumuisha "sekta ambayo inaunda ajira, uwezeshaji wa kiuchumi ndani ya jamii," Sani alisema.
Tamasha "limekua na kuwa maarufu hadi majimbo mengi ya kaskazini mwa Nigeria sasa yanaifanya, ikiwa ni pamoja na Jimbo Kuu la Shirikisho la Abuja kama sherehe," aliongeza.
Sherehe za Durbar zinaungana na alama nyengine za kitamaduni za Nigeria kwenye orodha ya urithi wa UNESCO, ikijumuisha mandhari ya kitamaduni ya Sukur ya kaskazini mashariki karibu na mpaka na Kameruni na shamba takatifu la Osun-Osogbo kusini mwa Nigeria.