Shambulio la roketi katika mji mkuu wa Somalia laua takriban watu 3

Shambulio la roketi katika mji mkuu wa Somalia laua takriban watu 3

Kundi la kigaidi la Al-Shabaab ladai kuhusika
Picha ya maktaba ( Sadak Mohamed - Shirika la Anadolu )

Takriban watu watatu waliuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika shambulizi katika mji mkuu wa Somalia Jumanne kwa roketi, alisema afisa mmoja.

"Shambulio hilo lilifanywa kwa roketi. Washambuliaji walitumia njia isiyo ya kawaida kurusha roketi hizo na zilirushwa kutoka viunga vya Mogadishu. Roketi moja ilianguka kwenye nyumba ya raia na kuua wanafamilia watatu akiwemo baba,” alisema msemaji wa polisi wa Somalia Meja Sadiq Aden Ali Doodishe, ambaye alizungumza kwa njia ya simu na Anadolu.

Takriban wengine wawili walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Doodishe alisema polisi hawajatambua lengo la shambulio hilo lakini wamemkamata mshukiwa mmoja baada ya operesheni iliyofanywa na vikosi vya usalama.

Chuo cha Polisi cha Kahiye cha Somalia na afisi zingine za usalama ziko karibu na mahali ambapo roketi hizo zilitua.

Vyombo vya habari vinavyowasiliana na kundi la al-Shabaab viliripoti kwamba lilidai kuhusika na shambulio hilo na kusema lililenga ikulu ya rais wa Somalia huko Mogadishu, ambayo hapo awali imekuwa ikilengwa na al-Shabaab kwa mashambulizi ya makombora.

Al-Shabaab imezidisha mashambulizi yake nchini humo, yakilenga walinda amani wa Umoja wa Afrika na wanajeshi wa serikali ya Somalia tangu Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kutangaza "vita vya kila namna" dhidi ya kundi hilo la kigaidi mwaka jana.

AA