Hifadhi ya Taifa Serengeti ya nchini Tanzania imeshinda tuzo ya Hifadhi Bora Afrika (Africa’s Leading National Park 2024) kwa mara ya sita mfululizo.
Hifadhi hiyo ambayo imejizoelea umaarufu mkubwa duniani kwa tukio la uhamaji wa nyumbu, imeshinda tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika kwenye ufukwe wa Diani nchini Kenya, usiku wa Oktoba 18, 2024.
Serengeti imezipiku zingine kwa ubora barani Afrika, zikiwemo Maasai Mara ya Kenya, Kruger ya Afrika Kusini, Central Kalahari ya Botswana na Kidepo Valley ya nchini Uganda.
Mafanikio hayo, yanaifanya Hifadhi ya Taifa Serengeti kushikilia tuzo hizo maarufu kama ‘‘World Travel Awards’ kuanzia mwaka 2019 hadi 2024.
Tuzo hizo zilitolewa na taasisi ya World Travel Awards, usiku wa Oktoba 18, 2024 katika ukumbi wa hoteli ya Diamonds Leisure Beach and Golf Resort iliyoko nchini Kenya.