Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Antalya
Nchi za Kiafrika zinazoshiriki katika kongamano la Diplomasia la Antalya mjini Antalya Uturuki zinataka kuwepo kwa mbinu zaidi za kidiplomasia katika masuala ili kuleta utulivu duniani.
"Diplomasia ni muhimu sana kwa mataifa yetu," Leonard Boiyo balozi wa Kenya nchini Uturuki anaiambia TRT Afrika.
"Kwa mfano, Kenya ina jukumu muhimu katika aina tofauti za diplomasia, tumechangia kwa muda mrefu katika eneo hili na kwingineko. Tumekuwa tukichangia katika mipango ya kulinda amani na ni kwa sababu hii ndiyo maana Kenya imepwewa mamlaka ya kuongoza usaidizi wa kimataifa wa usalama nchini Haiti kutokana na matatizo ya sasa yanayoendelea huko,” Boiyo anaongeza.
Mkutano wa Diplomasia la Antalya au Antalya Diplomacy Forum, hufanyika kila mwaka. Huu ni mwaka wa tatu na mkutano huo unafanyika kuanzia tarehe moja hadi tatu Machi, chini ya mada: "Kuendeleza Diplomasia katika Nyakati za Machafuko."
Imezipa nchi tofauti fursa ya kuongea wazi wazi kuhusu changamoto halisi zinazoathiri maendeleo yao.
Vikwazo vinakandamiza maendeleo
"Ikiwa tunazungumzia miundombinu, elimu na maendeleo katika teknolojia wakati watu wanaishi chini ya umaskini, haina maana,” amesema Peya Mushelenga, Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Jamhuri ya Namibia.
Sudan Kusini imepaza sauti yake ya kutaka Umoja wa Mataifa kuacha kutumia vikwazo dhidi ya mataifa maskini, ikisema kuwa inawalazimisha kutoendelea.
"Kuna baadhi ya mashirika ambayo yanavutiwa na vikwazo na yanatumia Umoja wa Mataifa," Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Peter Morgan ameiambia TRT Afrika.
Mnamo 2023, Umoja wa Mataifa uliongeza vikwazo kwa mwaka mwingine juu ya Sudan Kusini. Vikwazo hivyo ni pamoja na kufungia watu kadhaa mali, marufuku ya kusafiri na vikwazo vya silaha.
Sudan Kusini inapinga vikwazo ikisema inailazimisha isiendelee.
"Kwetu tunahisi kama UN inapaswa kuleta ustawi duniani kwa sababu ndiyo sababu imeundwa. Hofu ya vita vya pili vya dunia inapaswa kuendelea kukumbusha UN kwamba iliundwa ili kuweka ulimwengu wa amani, "Morgan anaongeza.
Sudan ambayo imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa ndani tangu Aprili 2023 imetoa hakikisho kwa Jukwaa kwamba bado imedhamiria kuamaliza vita nchini humo.
Mapigano kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF, tayari yamesababisha mzozo wa kibinadamu na kulazimisha zaidi ya watu milioni nane kukimbia makwao.
Takriban wakimbizi milioni 1.5 wametafuta hifadhi katika nchi jirani, kama vile Chad, Misri na Sudan Kusini.
"Bado tumejitolea kufanya amani, vita havitafanikisha chochote, nakubaliana na kauli mbiu ya diplomasia ya kongamano hili , diplomasia ni muhimu zaidi." Ali Elsadig Ali Hussien, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Sudan amesema.
Mkutano huu wa kimataifa umeangazia hitaji la juhudi za pamoja katika kukabiliana na ukosefu wa usalama.
"Ugaidi sio tu suala la Afrika, ni suala la kimataifa, ikiwa tunataka kukabiliana nalo ni lazima tufanye duniani kote; kama sivyo, hatuwezi kufanikiwa," Verónica Nataniel Macamo Dlhovo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano, Jamhuri ya Msumbiji imesema.
Umoja wa Afrika, pia unashiriki katika Mkutano wa Diplomasia wa Antalya.
"Kuna mgogoro mkubwa unaoendelea dunaini, tunaona masuala nchini Ukraine, Palestina, lakini pia ndani ya bara letu la Afrika tuna changamoto za amani na usalama katika baadhi ya nchi," Bineta Diop mjumbe maalum wa AU kuhusu amani na usalama wa Wanawake anaiambia TRT Afrika.
“Swali kubwa ni jinsi gani wanawake wanaweza kuchangia suluhisho? Na hayo ndiyo tunajadili hapa Antalya, "Diop anaongezea, "kwa hivyo ombi langu ni kwamba tunapaswa kuwa na hatua za pamoja ambazo tunaweza kutekeleza.”
Diop anapendekeza kwamba kila nchi inapaswa kuwa na uwezo wa kujipa kigezo cha jinsi ya kutekeleza majadiliano yanayofanywa katika Mkutano wa Diplomasia wa Antalya.
"Tunapaswa kujitathmini na kusema, tumefanya nini ili kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anaendeleza ajenda ya amani na usalama ya wanawake na kutoa taarifa kwa vitendo kuhusu kile ambacho tumefanya kupima maendeleo kuangalia changamoto?" anaiambia TRT Afrika.
"Kwangu mimi mkutano wa Antalya Diplomacy Forum ni Jukwaa zuri na bora sana, mwaka ujao tunahitaji kuwajibika zaidi,” Diop amesema.