Mwaliimu Nyerere akiwa na Mzee Mwinyi kaitka moja ya vikao. 

Mzee Ali Hassan Mwinyi, ambae amewahi kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili wa Tanzania, akichukua kijiti cha uongozi kutoka kwa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1985.

Mzee Mwinyi miongoni mwa simulizi zake nyingi, moja wapo ambayo siku zote inavuta hisia za wasikizaji ni ile ya Waziri mwenzake alipomfurusha katika nyumba ya serikali Oysterbay ambapo alikuwa anaishi na hatimae kumchukulia vifaa vyake vya ujenzi.

Mzee Mwinyi anasema, alikuwa anaishi katika nyumba ya serikali Oysterbay kama Waziri, wakati huo akiwa anajenga nyumba yake Mikocheni. Alikuwa ameweka vifaa vyake vya ujenzi nyumbani kwake Oysterbay, katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, nyumba hiyo akapangiwa waziri mwengine.

Rais Mwinyi anasema, "Waziri mpya alikuja nyumbani na kutaka nimpishe mara moja. Niende kwetu Zanzibar. Sikutaka ugomvi, nikajiondokea na kumuachia nyumba, pamoja na vifaa vyangu vya ujenzi akavichukua, nami sikumdai, nilipokuwa Rais, huyu bwana alikuwa na wasiwasi sana, ila nikaendelea kumpa uwaziri."

Mzee Ali Hassan Mwinyi akionyesha furaha ya ushindi. 

Urais wa Zanzibar na Muungano, mambo mawili ambayo hakuyategemea

Ali Hassan Mwinyi anasema katika kitabu chake kuwa alialikwa katika kikao cha CCM Dodoma, Januari, 1982, wakati huo akiwa Waziri na Mjumbe wa NEC lakini hakuwa mjumbe wa Kamati Kuu.

Anasimulia jinsi alivyokosa sehemu nzuri ya kulala alipokuwa Dodoama na hatimae kuishia katika chumba cha wanafunzi katika Chuo cha Biashara CBE, Dodoma.

Mzee Mwinyi, anasema, "Kikao hicho kilikuwa kigumu sana, kilipangiwa siku 5 lakini kilichukua siku 7. Kulikuwa na makundi mawili kutoka Zanzibar yaliyokuwa yakihasimiana sana. Kundi la kwanza lilijulikana kama wakombozi, na walinzi wa mapinduzi, kundi la pili likijiita 'front liners wa kuleta mabadiliko."

Anasema, "Wengine hatukuwa na kundi, kundi letu lilikuwa Zanzibar."

Front liners ndio walioongoza mashambulizi dhidi ya Rais Jumbe, hatimae Rais Jumbe akajiuzulu tarehe 29 Januari.

Nyerere alifurahi sana kuona uongozi wake umefikia kikomo baada ya Ali Hassan Mwinyi kushinda nafasi ya Urais wa Tanzania. Picha/Safari ya Maisha Yangu, Mzee Rukhsa. 

Baada ya Rais Jumbe kuachia nafasi ya urais Zanzibar, kitendawili kikawa, nani atachukua na kukaimu nafasi yake?

Wakati huo makundi mawili yakawa yanajipanga. Wakati huo huo, Mwalimu Nyerere nae alikuwa na mawazo mengine.

Mwalimu siku zote aliheshimu mawazo ya Sheikh Thabit Kombo, na mara zote alipenda kumsikiliza. Sheikh Thabit Kombo wakati mkutano huo ukiendelea alikuwa ameenda KCMC, Moshi kwa ajili ya matibabu. Mwalimu akamtumia ndege aletwe Dodoma haraka.

Alipofika Dodoma na kuulizwa kwenye kikao, Sheikh Thabit Kombo, bila kusita, akasema Ali Hasan Mwinyi. Rais Mwinyi, anakiri jinsi alivyoduwaa kwa jinsi uteuzi wake ulivyopokelewa kwa furaha na kila mmoja.

Rais Mwinyi anasema kuwa, baadae pia alikuja kubaini kuwa wazo la kumtafuta rais mpya asiye katika makundi na anaeweza kuunganisha Wazanzibar lilianza mapema zaidi tangu akiwa balozi Misri, na jina lake lilikuwa likiibuka mara kwa mara.

Wakati anakaimu NEC, ilikaa Machi 10, 1984, kujadili wagombea urais katika uchaguzi maalumu wa kumchagua rais wa Zanzibar. Yalipendekezwa majina mawili, na wote walikuwa hawakuomba. Sheikh Idris Abdulwakil aliomba kutoa jina lake kabla ya kupiga kura, likabaki jina la Ali Hassan Mwinyi.

Anasema, "Si haba sasa akawa Nzasa."

Jambo la pili. Dhana ya Rukhsa ilianza hapa. Ali Hassan Mwinyi na wenzake walipandisha mishahara ya wafanyakazi Zanzibar.

Wakaruhusu mambo yafuatayo:

Masharti ya wananchi kutembea wanavyotaka.

Wakazuia watu kukamatwa na kuwekwa ndani hovyo.

Wakaruhusu sekta binafsi kuingiza chakula nchini.

Na kuruhusu usafiri wa 'pick up' kubeba abiria maarufu kama 'chai maharage.

Mabadiliko haya, yaliwafurahisha wananchi wa Zanzibar.

Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Uteuzi wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Uteuzi wake ulipitia hatua tatu muhimu.

1. Mwalimu Kung'atuka na kutogombea tena

Tume mbili ziliundwa, moja ya serikali, na nyengine ya Chama kuchunguza na kushauri kuhusu jambo hilo. Wengi walitaka Mwalimu aendelee. Hata hivyo, kamati zote zilikubaliana kwa pamoja na mawazo ya Mwalimu ya kung'atuka. Mwalimu alifurahishwa sana na matokeo ya kamati zote mbili.

Mzee Ali Hassan Mwinyi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamen Mkapa (kulia).

2. Nani achukue nafasi yake?

Kwanza Mwalimu aliwaongoza wajumbe wa kamati kuu kubainisha sifa za mgombea anaetakiwa. Baada ya kukubaliana, hatua ya pili ilikuwa Mwalimu kama Mwenyekiti apendekeze majina matatu.

Usiku wa kuamkia siku ya mkutano maalumu, Agosti 15, 1985, mwalimu alikutana na wazee kutoka Zanzibar kupata maoni yao.

Rasi Mwinyi anasema, "Mkutano huo haukuwa mzuri, karibu wajumbe wote, walimtuhumu mgombea mmoja bila ushahidi, wala uthibitisho, kuwa ni Hizbu, msaliti, hasemi kauli ya Mapinduzi Daima."

Katika mkutano kesho yake Mzee Kawawa aliomba asijadiliwe, na hatimae akakubaliwa.

Ikiwa zamu ya Rais Mwinyi kujadiliwa, kwani alikuwa ni mwandamizi kama rais wa Zanzibar, na Makamu Mwenyekiti wa Chama. Wajumbe wote walimsifu Mwinyi, kisha Mwalimu akasema, "Kama hivyo ndivyo, basi hakuna haja ya kumjadili mwengine."

3. Kwenda kwa wapiga kura

Hatua ya tatu ilikuwa kwenda kwa wapiga kura, na katika uchaguzi mkuu mwa mwaka 1985, Ali Hassan Mwinyi alichanguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Pili, kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura.

"Mmoja wapo wa waliojawa na furaha alikuwa Mwalimu Nyerere akionyesha furaha ya kuhitimisha uongozi wake," anasema Mzee Mwinyi.

Mara tu alipoingia Ikulu, anasema, "Nilitangaza uteuzi wa kijana hodari kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, huyu ni Jaji Joseph Sinde Warioba."

Hii ilitokana na fikra nyingi na mashauriano na Mwalimu. Ingawa anakiri kwamba, jambo lililomsumbua kidogo ilikuwa ni kuhusu Salim Ahmed Salim ambae alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa pili wa Rais katika serikali iliyopita. Baada ya kushauriana na Mwalimu, aliamua kuunda nafasi ya naibu waziri mkuu ili impe heshima anayostahili.

Usikose kusoma makala inayofuata ambayo tutaangalia changamoto aliyokumbana nayo Rais Mwinyi katika kuivusha Tanzania kisiasa na kiuchumi wakati ambapo alinukuliwa akisema, "Nimepewa nchi kama papai bovu."

TRT Afrika