Rais Ali Hassan Mwinyi, alipoingia madarakani na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anakiri kwamba, alikabidhiwa nchi ikiwa inapitia katika mikondo miwili ambayo yote ililazimu mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa.
Ingawa Rais Mwinyi anakiri kwamba, kazi ya mageuzi ya uchumi haikuwa nyepesi, lakini anasema kuwa, mageuzi hayo yalikuwa ni lazima yafanyike kwa faida ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Hii ilitokana na kuchafuka kwa hali ya uchumi wa nchi kwa zaidi ya muongo mmoja. Rais Mwinyi anasema, "Sera, utekelezaji wa siasa za nchi hasa operesheni maduka, operesheni vijiji, mfumo wa mashirika ya umma, yaliyokuwa yanachechemea kwa kujiendesha kwa hasara na kuhitaji ruzuku kubwa, sheria za nguvu kazi, vyote vilichangia kupunguza uzalishaji. Pia bei duni za mazao, uhaba wa bidhaa za kila aina, uhaba wa mafuta na chakula, na hatimae ulanguzi na rushwa. Sheria zilipitishwa Machi 1985 kuwakamata wahujumu uchumi."
Rais Mwinyi anasema kulikuwa na uchumi wa aina mbili sambamba. Uchumi rasmi wa serikali usio na fedha na, uchumi wa ulanguzi na magendo wenye fedha ambao ulilea rushwa.
Mzee Rukhsa anaendelea kusema kuwa, hali hii pia ilichangiwa na Benki ya Dunia, mfumko wa fedha wa kimataifa na mataifa kadhaa ya magharibi yaliyoshinikiza kutimizwa kwa masharti ambayo Mwalimu Nyerere aliyaona kama ni kisiasa.
"Si wengi wa kizazi cha sasa, wanaojua kuwa ni Mwalimu Nyerere aliyekubali, japo kwa shingo upande kuwataka wazazi na walezi wachangie gharama za elimu,"anasema Mzee Mwinyi.
Mara tu baada ya kuanzisha uongozi, Mwalimu aliitisha kikao cha Kamati Kuu za Zanzibar. Katika kikao kile Mwalimu aliweka bayana kwamba, yeye tayari ameng'atuka hivyo kuutaka uongozi uliopo madarakani kuendelea na mazungumzo na wahisani ili ufikie makubaliano kwa sababu hali ya uchumi wakati huo ilikuwa ni mbaya sana.
Baada ya hapo, ndio yakafuata mageuzi ya kulegeza masharti ya biashara na uwekezaji.
"Sera, utekelezaji wa siasa za nchi hasa operesheni maduka, operesheni vijiji, mfumo wa mashirika ya umma, yaliyokuwa yanachechemea kwa kujiendesha kwa hasara na kuhitaji ruzuku kubwa, sheria za nguvu kazi, vyote vilichangia kupunguza uzalishaji. Pia bei duni za mazao, uhaba wa bidhaa za kila aina, uhaba wa mafuta na chakula, na hatimae ulanguzi na rushwa. Sheria zilipitishwa Machi 1985 kuwakamata wahujumu uchumi."
Mzee Mwinyi anasema, mkondo wa pili, ulikuwa ni mageuzi ya kisiasa, ambao ulikuwa mgumu zaidi.
Anasema, kwanza kabisa, Mwalimu Nyerere alikuwa aachie ngazi ya uenyekiti wa CCM mwezi Oktoba 1987, lakini kadri siku zilivyokaribia yalizuka mashaka na minong'ono, wapo waliojiona ndio wahimili wa ujamaa, ambao waliona hawezi Rais Mwinyi kuaminika kuulinda ujamaa, kwa sababu walidhani anaushabikia ubepari.
Wapo wengine waliodhai kuondoka kwa mwalimu itakuwa fursa kwao kuchukua madaraka, kwani rais Mwinyi asingeweza kuwadhibiti na anasema, "Walianza kujipanga."
Ili kukata mzizi wa fitina, Rais Mwinyi anasema, Oktoba, 1987 alipendekeza Mwalimu Nyerere aendelee kubaki kama mwenyekiti wa chama, na Mwalimu akakubali.
Lakini Rais Mwinyi anasema juhudi za wahafidhina hazikuishia hapo, kwenye mkutano huo wa Kizota, iliwasilishwa programu ya miaka 15 ya Chama ambayo haikuzingatia mageuzi ambayo tulikusudia kuyafanya.
Hii ilijenga taswira ya kuwa Chama na Serikali hazikuwa na mwelekeo mmoja.
Rais Mwinyi anasema kuwa, katika mkutano huo huo, msaidizi wake wa karibu, ambae alikuwa ni Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango, Mzee Cleopa Msuya, hakuchaguliwa kuingia kwenye kamati kuu ya CCM.
Rais Mwinyi anasema, "Kwa hili, wafaidhini wa ujamaa walinifunga goli, lakini hatimae hawakushinda mchezo."
Pili lilizuka swali la kubadili mfumo kuingia kwenye mfumo shindani wa vyama vingi, kwa ujumla viongozi wote pamoja na Mwalimu, tuliridhika na kufurahishwa na mchakato wa mapendekezo. Tulishindana na Mwalimu, kwenye jambo moja tu, la wagombea binafsi. Yeye alitaka wawepo, lakini wengi kwenye chama, na serikali, walihofu kwa haki kabisa kuwa hiyo itakuja kudhoofisha chama cha CCM, pale wasiopita kwenye mchujo wakiamua kusimama kama wagombea binafsi.
"Tulijitahidi kufanya iwe vigumu kwa vyama kuungana tukasema wakitaka kuungana lazima, wajifute kwanza kisha kuanza usajili upya."
Changamoto za Urais
1. Suala la kulifanyia marekebisho maadili ya uongozi-maarufu Azimio la Zanzibar.
Suala hili liliibuliwa na Mwalimu mwenyewe, akiwa bado mwenyekiti. Mwalimu alimuomba comrade Kingunge Ngombale-Mwiru aandae mada kuhusu hilo, na alipoiwasilisha, alishambuliwa sana, lakini rais Mwinyi anasema, "Comrade Ngombale alikuwa amejiandaa vizuri na aliwagonga sana waliopinga mabadiliko."
Alisisitiza kuwa, mali si haramu, kilicho haramu ni jinsi mali ilivyopatikana.
Hatimae, wajumbe wakakubali hoja ya mabadiko, na Kingunge akaombwa aifanyie kazi hoja ya mabadiliko, na kuiwasilisha tena NEC.
Mwalimu alistaafu uenyekiti wa CCM Oktoba 1990. Hivyo, mada ilipowasilishwa tena, rais Mwinyi anasema, "Zigo lilinikuta mimi ndio mwenyekiti."
Mabadiliko ya Zanzibar yalipokelewa kwa furaha na wajumbe wengi.
Swali la pili lilikuwa ni Muungano. Tume ya Jaji Francis Nyalali ilikuwa imeibua hoja, kuwa tukiingia kwenye mfumo wa vyama vingi basi tuwe na serikali ya shirikisho yenye serikali tatu, hoja hii ilikataliwa, ila baadae ikaunganishwa na hoja ya kumpata mgombea wenza wa rais wa Jamhuri ya Muungano iliyofanyiwa kazi na jaji Bomani.
Mara misuguano hiyo ikazaa kikundi kilichojiita, G55 kilichotaka serikali ya Tanganyika. Hii ilijidhihirisha katika kikao cha bunge cha bajeti cha mwaka 1992/93, Agosti 24. Rais Mwinyi anasema, "Yaliyotokea Bungeni, yaliniweka mahali pagumu sana. Sitasahau wabunge walipopitisha Azimio kwa kauli moja, kuhusu serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano."
"Katika kile ninachokiona sasa kama ulevi wa hisia, kuwa kuna wale walioweza kudhani watampuuza Mwalimu na lolote lisitokee. Wengine hasa walifikiri wameshampiga Mwalimu Nyerere bao la kisigino. Na walitaka tuamini kuwa maji yameshamwagika. Lakini Mwalimu hakukubali. Alijenga hoja, tena na tena, na kulaani kitendo kile. Na hatimae Mwalimu alifanikiwa."
Hatimae katika kikao cha Julai 29, 1994, NEC ilitoa azimio lililoweka wazi msimamo wa Chama cha Mapinduzi na kulimaliza jambo hili.
Rais Mwinyi anasema, "Katika mambo nayajutia katika uongozi wangu, ni kuliachia jambo hili likatokota hadi kufikia azimio la Bunge."
Katika kitabu chake, Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania, Rais Mwinyi anakumbuka jinsi alivyokosolewa na Mwalimu.
Jambo jengine, lililomuudhi sana Mwalimu ni kile alichokiita "Woga wa viongozi."
Rais Mwinyi anamnukuu Mwalimu aliposema, "Kukubali kufanywa vikaragosi wa viongozi ni dalili ya woga, si dalili ya heshima, kujenga mazoea ya kutii viongozi hata katika mambo haramu, ni dalili ya woga, ni kukaribisha udikteta."
Rais Mwinyi anamalizia kusema kuwa, Mwalimu aliandika kitabu kile la lugha kali na ghadhabu kubwa, sasa anasema, mfikirie yeye, aliyekaa na Mwalimu faragha na akayapokea hayo, kwa ukali na ghadhabu ile ana kwa ana.
Swali la tatu ni OIC, moja ya hoja zilizozaa kundi la G55 ilikuwa suala la Zanzibar kujiunga na Jumuia ya Ushirikiano wa nchi za Kiislamu OIC.
Rais Mwinyi anarudia kusema kuwa sababu ya kujiunga haikuwa mambo ya dini, bali umaskini tu na matarajio ya misaada.
Tatizo lilikuja pale ambapo mwanasheria mkuu wa serikali Damian Lubuva, kushauri kuwa haikuwa sahihi kwa Zanzibar kujiunga pekee, lakini Zanzibar iliomba uanachama kwa sira na kuongopa kuwa serikali ya Muungano iliridhia ombi hilo, bahati nzuri jambo hili liliisha salama kwa ushirikiano na bunge.
Nne, Rais Mwinyi anakiri kuwa, miongoni mwa mambo yaliyomsumbua na kumsikitisha sana kipindi cha uongozi wake, ni ugomvi na kufarakana ndani ya dini na madhehebu ya dini sambamba na tuhuma mvutano baina ya dini moja na nyengine.
Rais Mwinyi anasema, kilichomuudhi sana tena sana ni vile mambo hayo ya dini yalivyojipenyeza kwenye siasa, ukaenezwa uongo eti kwa kuwa mimi ni Muislamu basi serikali yangu inaunga mkono vitendo hivyo vya kihuni.
Pia ulienezwa uongo kuwa eti nilipendelea waislamu wenzangu kwenye uteuzi kwa nafasi mbalimbali. Lakini Machi 1993, Rais Mwinyi alianzisha Baraza la Ushauri kuhusu dini ili kujenga uelewano na kuzuia migogoro ya dini.
Tano Rais Mwinyi anabaini kuwa dhana yake ya Rukhsa pia iliwafikia wafanyakazi kwa kuruhusu vyama huru vya wafanyakazi, lakini ndani ya miaka miwili, ya kuanzishwa, COTU, waliunga mkono migomo mikubwa, kwa walimu na baadae wakaitisha mgomo wenyewe Machi 1-3.
Rais Mwinyi anakiri kuwa, kwa ujumla, alianza vizuri sana wa wafanyakazi, ila alikuja kumaliza vibaya sana nao.
"Moja wapo ya mambo, yaliniuma sana, ni mauaji ya wafanyakazi wanne, na kujeruhiwa vibaya wengine 16 wakati wa mgogoro juu ya maslahi huko Kilombero, lakini hatua mbalimbali zilichukuliwa na serikali baada ya mkasa huo."
Rais Mwinyi anasema, kipindi chake cha pili, mwaka 1990-1995 kiligubikwa na mivutano mikubwa zaidi, na kutokufahamiana baina ya serikali na vyama vya wafanyakazi. Anasema, Na wengine kwa kweli walinikera na kuniudhi sana, wakiwemo walimu."
Pamoja na juhudi za kufikia muafaka, waliitisha mgomo na ikalazimika kuwadhibiti angalau kwa muda. Cotu nao waliitisha mgomo eti kwa sababu sikutekeleza ahadi niliyokuwa nimeitoa kwenye sherehe za wafanyakazi Mei Mosi 1993, ya kuongeza mishahara.
"Wafanyakazi walinishukuru kwa migomo, baada ya kupanua mipaka ya uhuru wao. Wakaninunia, kiasi cha kukataa kunialika kwenye Sherehe za wafanyakazi Mei Mosi zilizofuata, mwaka 1995, wakamualika Mwalimu huko Mbeya, na Mwalimu akawakubalia," anasema Mzee Mwinyi.
Mwalimu alimsema sana, mimi na serikali yangu, na CCM kwa kuacha misingi ya Ujamaa na Azimio la Arusha. Pamoja na kubinafsisha mashrikia ya umma, wafanyakazi walifurahi sana tulivyosemwa pale Mbeya.
Wanafunzi wa vyuo vikuu na hawakuwa nyuma, huko Sokoine baadhi walikataa kulala 3 kwenye chumba kimoja, wakafanya fujo kubwa ikabidi kuwasimamisha masomo zaidi ya nusu ya wanafunzi.
Hapo chuo kikuu cha Dar es Salaam, ilibidi niwarudishe makwao wanafunzi Mei 12, 1990 mpaka Januari, 1991, hii ilifuatia kukataa kwao kuingia madarasani na kubandika makaratasi kwenye mbao za matangazo na maeneo mengine yakiwa na matusi ya kila aina, dhidi yangu binafsi, na serikali.
Rais Mwinyi anasema, "Kwa kweli wanafunzi wale walituvunjia heshima kiasi ambacho nilishindwa kuvumilia."
Sita, na mwisho wa changamoto, Mwinyi anasema, "Moja wapo ya mambo yaliyonitikisha sana wakati wa urithi wangu ni kuibuka mjadala mkali kuhusu kinachoitwa uzawa, hasa kuanzia mwaka 1993, yakawepo maneno mengi, chuki, na uadui baina ya wafanya biashara wa kiafrika na wa kihindi.
Kwa upande wa mafanyabiashara wa kiafrika muhusika mkuu alikuwa hayati Reginald Mengi, ambae alipokea barua za vitisho kwa maisha yake na mali zake, na ilibidi apewe ulinzi. Mchochezi mkuu alikuwa Reverend Hayati Christopher Mtikila.
Ilisitikisha sana, ushindani mkali baina ya wafanyabiashara ulipogeuka kuwa uadui kwa msingi wa ubaguzi wa rangi, dini na ukabila.
Rais Mwinyi anasema, alifanya juhudi kubwa kukemea jambo hilo na pia kuchukua hatua madhubuti za kulinda watu na mali zao.