Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliongoza Serikali ya Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Novemba 5, 1985.    

Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliongoza Serikali ya Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Novemba 5, 1985. Alipokea uongozi kutoka kwa Julius Nyerere. Mzee Rukhsa alizaliwa Kivule, Mkuranga, mkoa wa Pwani Mei 5, 1925.

Alikuwa ni mtoto wa kiume pekee katika watoto watano, waliozaliwa na mzee Hassan Mwinyi Magondi pamoja na mama yake Aisha Mwinyi Shehe. Wote, kwa muda mrefu, walikuwa wakiomba kupata mtoto wa kiume, ambae hatimae walimpata.

Katika kitabu chake cha 'Mzee Rukhsa, Safari ya Maisha Yangu,' Mzee Mwinyi, anasimulia jinsi kuzaliwa kwake kulivyokuwa furaha na faraja kwa wazazi wake.

"Sijawahi kukopa katika maisha yangu."

Ali Hassan Mwinyi

Ni kutokana na sababu hiyo, ndipo alipozaliwa tu, baba yake, alimpachika jina la 'Si Haba' likionyesha kutimia kwa kiu chake cha kupata mtoto wa kiume na kumshukuru Mungu kwa dua yake kujibiwa.

Mzee Mwinyi pia, amewahi kusimulia katika kitabu chake, chenye kurasa 491 kuwa, baba yake pia amewahi kumpachika jina jengine la Nzasa, likiwa na maana sehemu ya ardhi ambayo haikauki maji, sehemu ambayo daima inakuwa na unyevunyevu, chepe chepe au tepetepe.

Na jina hilo, anakiri kwamba, limekuwa sehemu ya baraka na mafanikio katika maisha yake. Na kuthibitisha hilo, mwenyewe anasema, "Sijawahi kukopa katika maisha yangu."

Safari ya kwanza

Akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 4, mwaka 1929, yeye na baba yake walisafiri na kwenda Zanzibar ambapo walifikia nyumbani kwa Mzee Suwedi bin Mgeni, ambae alikuwa rafiki wa chanda na pete wa baba yake Ali Hassan Mwinyi. Lengo la safari yao, lilikuwa ni kwenda kuanza masomo, chini ya uangalizi au ulezi wa Mzee Suwedi. Hiyo ndio ilikuwa safari yake ya kwanza maishani mwake, lakini pia, ilikuwa ndio ufunguo wa safari zake nyengine zote katika maisha yake ya zaidi ya miaka mia moja.

Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa na wajukuu wake. 

Akiwa chini ya uangalizi wa Mzee Suwedi, alianza kwenda shule, na kusoma masomo ya dini, yani Qur'an. Lengo lake kubwa, alitaka baadae kuwa sheikh.

Baada ya kuhitimu masomo katika Chuo cha Qur'an kilichopo Manga Pwani, Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi alijiunga na shule ya msingi akiwa na umri wa miaka nane na nusu. Januari, 1937, pamoja na mwanafunzi mwengine, walikuwa ni wanafunzi pekee kutoka darasani kwake kuchaguliwa kwenda darasa la 5 Shule ya Kata Dole.

Katika simulizi yake, Mzee Mwinyi anasema kuwa, hapo kwa mara ya kwanza ndipo alipoanza kushuhudia ubaguzi wa rangi baada ya kuona wanafunzi wa kiarabu wakiishi katika bweni pekee yao.

Kati ya mwaka 1943-1944, alisomea kozi ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Dole, na wakati huo, kiwango hicho cha elimu kilionekana kuwa ndicho kikubwa zaidi katika eneo hilo. Hata hivyo, baadae alihamishwa na kupelekwa Bumbwi.

Mwaka 1954, safari yake ya kujenga maisha iliendelea, hasa baada ya kupata fursa ya kwenda nchini Uingereza kubobea zaidi katika fani ya ualimu. Masomo yake yaliendelea mpaka mwaka 1956. Miaka saba baadae alipelekwa tena nchini Uingereza kusoma katika Chuo Kikuu cha Hull. Hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 1961 na 1962.

Mwaka 1962 akarudi nyumbani na kuteuliwa kuwa mkuu wa Chuo cha Ualimu.

Maisha ya Kazi na Utumishi wa Umma

"Wengi wetu tulikuwa hatuna uzoefu wa kazi tulizopewa, tukaambiwa jifunzeni humo humo. Tukachechemea, lakini upepo wa ari na matumaini ukajaa katika taifa, jahazi la utumishi wa serikali likasafiri."

Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili Tanzania

Mzee Mwinyi anasimulia kuwa, upepo wa Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964, yaliyoondoa utawala wa waarabu, hayakumuacha salama. Ni wakati huo ambapo anasema, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Elimu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

"Wengi wetu tulikuwa hatuna uzoefu wa kazi tulizopewa, tukaambiwa jifunzeni humo humo. Tukachechemea, lakini upepo wa ari na matumaini ukajaa katika taifa, jahazi la utumishi wa serikali likasafiri," anasimulia Mzee Mwinyi katika kitabu chake.

Simu ya Ikulu: Tamaa ya Kupata, Hofu ya Kukosa

Mzee Mwinyi akiwa na umri wa miaka 45, nyota yake ya uongozi ikiwa tayari imeanza kuchomoza. Pasina matarajio yoyote, mwaka 1970, alipokea simu ya kuitwa Ikulu na rais wa wakati huyo ambae alikuwa ni Mzee Amani Abeid Karume. Baada ya muda kidogo, akaona gari la polisi limekuja kumfuata. Khofu ya kutojua anachoitiwa ikamtawala.

Kutokana na hilo, alikataa kuingia kwenye gari ya polisi na kuwaambia, kwa sababu yeye sio mfungwa wala mtuhumiwa, basi atakwenda mwenyewe.

Alhaj Ali Hassan Mwinyi rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maarufu Mzee Rukhsa. 

Kukashuhudiwa vuta nikuvute kati yake na polisi. Ikabidi gari ya polisi imfuate hadi Ikulu. Anasema, alipofika Ikulu, kwanza alijipa muda kidogo wa kupumzika na kujifuta jasho usoni pamoja na miguuni, na kukusanya pumzi. Lakini yote hayo hayakusaidia kuondoa hofu iliyokuwa imetawala moyoni mwake, fikra za kila aina zilitawala kwani hakujua anachoitiwa, na iwapo atakuwa salama au la.

Hatimae akaenda kumsalimu rais Karume.

Rais Karume, ambae alikuwa na sauti ya ubabe alikuwa na machache ya kumuambia.

"Rais Nyerere ameomba majina mawili, ili kati ya hayo, mmoja amteuwe kuwa waziri, jina lako lilikuwa moja wapo. Hivyo sikiliza taarifa ya habari saa mbili usiku."

"Moyo wangu ulijaa mchanganyiko wa uoga na furaha isiyoeleza, tamaa ya kupata, na hofu ya kukosa," anasimulia Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Usiku huo Mzee Rukhsa aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais.

"Nililala mwalimu, nikaamka Waziri katika serikali ya Muungano," anasema.

Hapo Mzee Rukhsa anakiri kwamba, ndio ulikuwa mwanzo wa yeye kukutana na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Mzee Mwinyi anasema, alikaa mwaka mzima bila kupangiwa shughuli maalumu, hivyo uwaziri wake ulikuwa bila shughuli rasmi.

"Nililala mwalimu, nikaamka waziri katika serikali ya Muungano."

Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mwaka uliofuata, ambao ni 1972, Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya, nafasi ambayo alidumu nayo hadi 1975. Ingawa mwaka huo hakugombea katika uchaguzi, lakini Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Uwaziri wamtumbukia nyongo

Miaka miwili tu baada ya uteuzi huo, mwaka 1977, Mzee Mwinyi alijikuta katika hali ambayo sio ya kawaida.

Katika Mikoa ya Mwanza na Shinyanga, kulitokea mauaji na vitendo vya mateso yaliyofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama dhidi ya wananchi. Mauaji hayo baadae yalikuwa kupewa jina la 'Mauaji ya Mwash.'

Ingawa Mzee Mwinyi hakuhusika na mauaji hayo, lakini kama Waziri aliyepewa dhima ya Ulinzi na Usalama wa nchi, alijikuta hana budi bali kuwajibika.

Mzee Mwinyi anasema kuwa, uamuzi huo haukutokana na shinikizo la mtu yeyote bali ulikuwa uamuzi wake binafsi.

Sehemu ya mwisho ya barua yake ya kujiuzulu, inayotoka kwake kwenda kwa Nyerere ambae ndie aliyekuwa na mamlaka ya uteuzi wakati huo, inasema.

"Kisiasa mzigo huu ni wangu na nakubali kuubeba kwani hakuna mwingine wa kuubeba. Kwa hiyo Mwalimu, nakuomba mambo matatu. Kwanza, naomba radhi mimi nafsi yangu na pia naomba radhi kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu katika kosa hili. Tatu, kwa fedheha hii, naomba unikubalie nijiuzulu Mwalimu."

Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa na familia yake. 

Hatua hii ya Mzee Mwinyi, na ujasiri aliouonyesha wakati huo, ulikuwa kigezo cha uongozi uliotukuka. Wengi mpaka leo, wanapigia mfano hatua hiyo, ya uwajibikaji.

Ni kutokana na hatua hiyo, mwaka mmoja baadae, 1978, mpaka Oktoba 1981, Mzee Mwinyi aliteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika ubalozi wake huko nchini Misri. Baadae aliteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, na hatimae kuteuliwa tena katika nafasi yake ile ya mwanzo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais. Lakini baadae alipewa nafasi kubwa zaidi ya kuwaongoza wananchi, ambayo ni kuwa Rais wa tatu wa Zanzibar (1984-1985) na Rais wa pili wa Tanzania.

Inaendelea

Chanzo: Mzee Ruksa, Safari ya Maisha Yangu, Ali Hassan Mwinyi (2020)

TRT Afrika