Na Sylvia Chebet
Baada ya karne moja ya kusubiri, hatimaye, mwenge wa Olimpiki umefika nchini Ufaransa, jiji litakalokuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki kwa mwaka 2024.
Mwenge wa mashindano hayo kwa mwaka huu uliwashwa katika eneo la Olympia, ambapo ndio kitovu cha michezo hiyo katika Ugiriki ya kale, siku ya Aprili 16, ikiashiria hitimisho la maandalizi ya miaka saba ya michezo hiyo itakayoanza Julai 26.
“Mwenge wa Olimpiki ni ishara kubwa mno kwenye michezo hii,” Martin Keino, mwanariadha maarufu aliyevunja rekodi saba katika riadha anaiambia TRT Afrika.
“Huashiria kuanza kwa tukio kubwa la kimchezo duniani, linaloleta wanamichezo bora kabisa.”
Akivaa uhusika wa kuhani wa kike, muigizaji wa Ugiriki Mary Mina alimuwashia bingwa wa mchezo wa kupiga kasia wa Ugiriki Stefanos Ntouskos.
Baada ya mbio fupi, alimkabidhi Laure Manaudou, kama mwenyeji wa mashindano hayo.
“Hakika ni heshima kubwa kuwa mfaransa wa kwanza kubeba mwenge huu,” Laure amesema Manaudou.
"Hii ni muhimu zaidi kwangu kwani nina uhusiano mkubwa na nchi hii ambapo safari yangu ya michezo ilichukua mkondo mzuri. Ishara hii huleta kumbukumbu na hisia nyingi. Ninajivunia kuiwakilisha Ufaransa katika hafla hii," aliongeza.
Baada ya kukimbizwa kwa siku 11 kote Ugiriki, mwali huo ulikabidhiwa kwa waandaaji wa Michezo ya Paris katika uwanja wa Panathenaic wa Athens, mahali pa Michezo ya kwanza ya kisasa mnamo 1896.
Kisha ukavuka Bahari ya Mediterania kwa meli ya nguzo tatu na kuwasili kwenye ardhi ya Ufaransa huko Marsaille mnamo Mei 8.
Mwenge huo umepangwa kusafiri kote nchini Ufaransa kwa siku 68, na kuhitimishwa na kuwashwa kwenye sherehe za ufunguzi wa Michezo hiyo mnamo Julai 26.
Mwenge huo umekuwa ni sehemu ya utamaduni katika michezo ya Olimpiki tangu michezo hiyo ifanyike katika jiji la Berlin mwaka 1936.
Tangu wakati huo, wanariadha mashuhuri (waliocheza au waliostaafu) na wenye mafanikio makubwa ya kimichezo wamepewa heshima ya kukimbia na mwenge wa Olimpiki na hivyo basi kuwa na heshima ya kuwasha kikombe cha Olimpiki kwenye sherehe za ufunguzi.
Wakimbiza mwenge 11,000 wanashiriki katika mbio hizo kutoka Ugiriki hadi Ufaransa, kwa mwaka huu.
Keino anakumbuka wakati wake kama mshiriki wa michezo ya Olimpiki ya Beijing, mwaka 2008.
"Ilikuwa ni jambo la kupendeza sana kushuhudia kijiti kikizunguka na kuwasha mwali wa Olimpiki," anasema.
Kulingana na Keino, kitu cha kipekee zaidi ni kuwa kinara wa tukio hilo.
"Alitunukiwa katika Olimpiki ya Rio 2016 na alikuwa wa kwanza kutoka Kenya na Afrika kufanya hivyo na kutunukiwa mwanzoni mwa michezo ya Olimpiki."
Keino, mwanariadha mashuhuri katika uwanja wa michezo wa Kenya, aliitangaza nchi hiyo kwa kipaji cha ajabu cha riadha kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka 1968.
"Ilikuwa jambo kubwa, heshima kubwa kwake kutambuliwa kwa njia hiyo."
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) Thomas Bach alisema kuwa moto huo ni ishara ya matumaini katika ulimwengu uliojaa hali ya kukata tamaa.
"Katika nyakati hizi ngumu tunazopitia, huku vita na mizozo ikiongezeka, watu wamechoshwa na chuki zote, uchokozi na habari mbaya wanazokabiliana nazo siku baada ya siku," Bach alisema katika hotuba yake.
"Tunatamani kitu ambacho hutuleta pamoja, kitu ambacho kinatuunganisha, kitu ambacho kinatupa matumaini. Mwenge wa Olimpiki ambao tunawasha leo ni ishara ya tumaini hili."
"Ndio tukio pekee linaloleta ulimwengu mzima pamoja katika mashindano ya amani," alisema na kuongeza: "Inawezekana kushindana vikali dhidi ya kila mmoja na wakati huo huo kuishi kwa amani pamoja chini ya paa moja."