türkiye

Tukur ni miongoni mwa takriban wanafunzi elfu 10, wengi wao kutoka Afrika, ambao wamenufaika na ufadhili wa masomo kutoka Uturuki katika kipindi cha miongo kadhaa.

Hii ni sehemu tu inayoonyesha ushawishi wa Uturuki na jinsi unavyogusa maisha ya watu katika bara la pili kuwa na idadi kubwa ya watu.

Mamia ya shule zinazofadhiliwa na Uturuki, zinafanya kazi katika mataifa mbalimbali barani Afrika-husaidia vijana wa kiafrika kupata elimu yenye ubora na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za ulimwengu kwa ujasiri unaotakiwa.

Ushawishi wa Uturuki barani Afrika hii leo, unahusisha sekta mbalimbali, huku Ankara ikiliunga mkono bara la Afrika kama sehemu yake ya sera za kigeni.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameiongoza nchi yake katika jitihada hizo, huku akisafiri katika nchi zaidi ya 30 katika miaka ya hivi karibuni barani Afrika na kutilia mkazo vipaombele vya serikali yake.

Pia amesaini makubaliano mbalimbali ya pamoja yenye lengo la kudumisha uchumi, siasa, tamaduni, elimu na mahusiano ya kijeshi.

Wachumbuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, idadi ya safari alizofanya Erdogan sio za kawaida kwa kiongozi yoyote, hii ni ishara tosha ya dhima aliyokuwa nayo ya kudumisha ushirikiano kati ya Uturuki na Afrika.

“Uturuki imekuwa na akili sana” katika kuisuka sera yake ya kigeni kwa Afrika na bara la Asia,” amesema mwanadiplomasia mstaafu kutoka Nigeria Sulaiman Dahiru.

“Uturuki ni nchi iliyoendelea, ina uchumi mkubwa, na ina msingi mzuri wa viwanda. Kwa hiyo, kusambazwa kwa viwanda vyake barani Afrika, itakuwa ni faida kwake na kwa Afrika,” ameiambia TRT Afrika.

Dahiru ana amini kwamba, uhusiano huo umekuwa na mafanikio kwa sababu Uturuki inafaidika kupitia soko kubwa la Afrika huku makampuni ya Uturuki yanayofanya kazi barani Afrika yanasaidia katika ukuaji wa miundombinu pamoja na ajira.

Ukuaji wa biashara

Takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki, zinaonyesha kwamba kiwango cha biashara kwa mwaka kati ya Uturuki na Afrika kimeongezeka kutoka dola za kimarekani bilioni 5.4 mwaka 2003 mpaka zaidi ya dola za kimarekani bilioni 34 mwaka 2021.

Makampuni ya kituruki pia yametekeleza miradi yenye thamani ya takriban dola za kimarekani bilioni 78 katika nchi mbalimbali barani Africa.

Baadhi ya miradi hiyo ni katika miundombinu, shule na misaada ya kibinadamu. Uturuki vile vile, ina makubaliano huru ya kibiashara na nchi kadhaa, kama vile Misri, Morocco, Mauritius na Tunisia.

Biashara ya bidhaa kutoka makampuni ya kituruki imeongezeka maradufu Afrika, hasa bidhaa za samani, nguo, magari na zana za kielektroniki, bila kusahau vyakula.

Mbali na hiyo, familia nyingi barani hivi sasa zinaagiza vyombo moja kwa moja kutoka Uturuki. Hii imerahisishwa zaidi na uwepo wa miundombinu mizuri ya mtandao na mfumo imara wa biashara.

Ishara nyengine ambayo iko dhahiri ya kukuwa kwa mahusiano ya kibiashara na uchumi ni ukuwaji wa idadi ya safari za ndege zinazofanywa na Shirika la Taifa la ndege yani Turkish Airlines katika mataifa mbalimbali ya bara la Afrika.

Uturuki pia imeongeza idadi ya balozi zake katika nchi za kiafrika, kutoka 12 had 44 katika kipindi cha miaka 20.

Kwa upande mwengine, nchi zaidi ya 28 za Afrika zimefungua balozi jijini Ankara katika kipindi cha muongo mmoja, hii kwa kiasi kikubwa imeongeza uhusiano wa kidiplomasia.

Uturuki pia, imechaguliwa kuwa mshirika muhimu na Umoja wa Afrika mwaka 2008 baada ya kupewa jukumu la kuwa mwanachama mwangalizi mwaka 2005. Viongozi wa Afrika, wamefanya mikutano kadhaa ya kimkakati na Uturuki.

Haya na utekelezaji wa sera ya Uturuki ya Ushirika na Afrika imesaidia kuhakikisha kuna ukuaji wa haraka wa kiuchumu, utamaduni, miundombinu pamoja na usalama na ushiriano wa masuala ya kijeshi.

Ushawishi bila shuruti

Idayat Hassan, Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia na Maendeleo, ambalo ni shirika huru linalokuza masuala ya amani, maendeleo na demokrasia Afrika Magharibi, anasema, “Uturuki imeweza kuteka nyoyo na akili za Afrika wengi kwa kutumia ‘ushawishi usio na mabavu.”

Mkakati wa Ankara wa kuwekeza katika fursa za elimu kwa waafrika, upatikanaji wa huduma za afya na mafunzo kwa watu mbalimbali wenye uweledi, huku wakiimarisha uhusiano wa watu kwa watu, na serikali kwa serikali, umekuwa na tija kubwa kwa watu wengi,” ameiambia TRT Afrika.

Filamu za Kituruki na vipindi vya televisheni, zinazotafsiriwa kwa Kiengereza na lugha nyengine mbalimbali ikiwemo Kiswahili, zimeonyesha mila na tamaduni za waturuki katika sebule za mataifa ya kiafrika.

Hassan anasema, kuimarishwa kwa mahusiano ya hivi karibuni ni mwendelezo mzuri kati ya Afrika na Uturuki tangu kuwepo kwa dola ya Ottoman.

“Wanachofanya sasa hivi Uturuki ni kupaka mafuta mahusiano hayo na kuyafanya yawe na uhalisia zaidi,” Hassan anasema.

Mbadala wa Magharibi

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Uturuki, nchi ina dhamira ya kushirikisha uzoefu wake wa kihistoria, kijamii, kisiasa na kitamaduni na wengine, pamoja na fursa na rasilimali zake na mataifa ya Afrika, kwa misingi ya, “Suluhu ya Africa kwa matatizo ya Africa.”

Wachambuzi wanahisi, hapo ndipo Uturuki ilipoweza kuteka nyoyo za mataifa ya Afrika.

“Uturuki inakuja kama mbadala wa mataifa ya magharibi barani Afrika,” anasema Hassan.

Mwanadiplomasia mstaafu Sulaiman Dahiru anasema kwamba, “Uturuki haiingilii masuala ya ndani ya nchi za kiafrika, tofauti na ilivyo kwa mataifa ya magharibi ambayo yanataka kushurutisha nini kifanyike na nini kisifanyike.”

Mataifa ya magharibi, ikiwemo Uingereza na Ufaransa, yametawala nchi nyingi za Afrika.

Lakini kwa miaka mingi, mataifa hayo hayakuwa wakweli na waaminifu katika mahusiano yao na Afrika,” na yamekuwa hayaisaidii Afrika inavyotakiwa licha ya kupora rasilimali zake,”ameongeza Dahiru.

“Ingawa ukoloni umeisha, lakini wanaiona Afrika kama bado ni koloni lake. Afrika sasa inakataa kuendeshwa,” ameiambia TRT Afrika, na kuongeza, “Malengo ya Afrika ni maendeleo na heshima. Uturuki inaiheshimu Afrika.”

Haya ni maoni yaliyotolewa na Idayat Hassan. “Mataifa ya magharibi hayako tayari kwenda na uhalisia wa bara la Afrika leo, kwa sababu sera ya Uturuki inakubalika barani Afrika.” Tukirudi Istanbul, Tukur anasubiri siku atakayokamilisha masomo yake.

Ni matarajio yake kurudi nyumbani na kuhamisha chochote alichojifunza kwa kizazi chengine za Afrika. Kijana huyu wa ki Nigeria, bila shaka atakuwa na sehemu ya Uturuki popote atakapokuwa.

TRT Afrika