Sababu ya Jeshi la Niger kusitisha mahusiano na Marekani imeibua mjadala kutoka kwa wachambuzi:Picha/ Rais wa Jamhuri ya Niger.

Na Abdulwasiu Hassan

Utawala wa kijeshi wa Niger umesitisha uhusiano wake na Marekani.

Hapo awali, wanajeshi wa Marekani na wafanyakazi wa kawaida waliruhusiwa kufanya kazi Niger, kufuatia mkataba uliotiwa saini kati ya nchi hizo mbili mwaka 2012.

Jeshi la Marekani limekuwa likiendesha kikosi cha anga katika mji wa Agadez, ulioko kilomita 920 kutoka mji mkuu wa Niamey, wakiutumia kurusha ndege zisizo na rubani na shughuli nyinginezo.

Kambi hiyo ambaye ilijengwa kwa gharama za dola milioni 100, ina vikosi vipatavyo 1000. Lakini katika siku za hivi karibuni, Niger imezidi kujitenga na nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na watawala wake wa zamani, Ufaransa , tangu kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi Julai mwaka jana.

Ziara ya wajumbe kutoka Marekani

Uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Niger haukuweza kusaidia nchi hiyo kutatua baadhi ya matatizo yake ya kiusalama, kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Malam Salissou Sa'adou, anayepatikana Niamey.

"Wamarekani wapo Agadez ambayo iko mbali na Tilleberi na Diffa ambapo mapigano yanaendelea dhidi ya magaidi na watu wenye itikadi kali. Kwa hiyo, sioni tatizo lolote kuwataka kuondoka nchini,” Sa'adou anaiambia TRT Afrika.

Uamuzi wa kusitisha uhusiano wa kijeshi na Marekani umekuja mara tu baada ya ujumbe wa kijeshi na kidiplomasia wa Marekani kuondoka nchini humo kufuatia ziara ya siku tatu bila kumuona kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdourahmane Tiani.

Naibu Waziri wa Afrika, Molly Phee na mkuu wa Kamandi ya Marekani na Afrika, Jenerali Michael Langley walikuwa ni sehemu ya ujumbe huo.

Kukiuka itifaki

Msemaji wa Jeshi la Niger, Kanali Amadou Abdramane alitangaza kusitisha uhusiano huo kupitia televisheni ya taifa.

Alisema uwepo wa wanajeshi wa kimarekani nchini humo ni kinyume na katiba, na ulifanywa kwa ridhaa ya upande mmoja mwaka 2012.

Alisisitiza kuwa ujumbe wa Marekani haukufuata itifaki za kidiplomasia wakati wa ziara hiyo kwani Niger haikuarifiwa kuhusu idadi na ukubwa wa ujumbe huo, tarehe na hata ajenda za mkutano.

Msemaji wa Jeshi la Niger, Kanali Ahmadou Abdramen, alitoa taarifa za maamuzi kupitia televisheni ya taifa.Picha/ Facebook/RTN

"Serikali ya Niger inalaani vikali tabia ya dharau inayoambatana na vitisho vya kulipiza kisasi kutoka kwa mkuu wa ujumbe wa Marekani kwa serikali na watu wa Niger," Kanali Abdramane alisema.

Mahusiano ya nchi hizo mbili yaliingia dosari baada ya tamko la Marekani kufuatia mapinduzi ya Oktoba 2023.

Licha ya uamuzi huo wa Niger, Molly Phee alisema kuwa Amerika inaweza kuendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa nchi hiyo. Hata hivyo, Marekani imeibua wasiwasi juu ya madai ya kuongezeka kwa uhusiano kati ya Niger na Urusi.

Kukua hisia dhidi ya Magharibi

Matokeo mapya nchini Niger yanaonekana kama ishara nyingine ya kuongezeka kwa hisia za chuki dhidi ya magharibi zinazoenea katika eneo la Sahel la Afrika kufuatia mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi katika nchi kadhaa zikiwemo Niger, Mali na Burkina Faso.

Mwaka jana, jeshi la Niger liliondoa majeshi ya Ufaransa, miaka michache baada ya kuondolewa Mali.

Takribani wanajeshi 1,500 waliondoka Niger nchini humo mwezi Januari baada ya wiki za maandamano ya raia.

Uhuru

Kumalizika kwa uhusiano wa kijeshi na Marekani hakuonekani tu kama kujiweka mbali na Magharibi, pia linaonekana kama kujipatia uhuru na mamlaka, Sa'adou anasema.

Wanajeshi hao walikata uhusiano wa kijeshi na Wamarekani katika jaribio la ''kukimbia ukoloni mamboleo'' alisema, akiongeza kuwa nchi inaonekana kujaribu kuepuka mataifa yenye nguvu duniani ambayo yamekuwa ''yakinyonya'' rasilimali zake.

Takribani wanajeshi 1,500 waliondoka Niger nchini humo mwezi Januari baada ya wiki za maandamano ya raia.Picha:Reuters

Mchambuzi huyo anaamini kuwa uamuzi wa Niger unaweza usiwe na athari kubwa kwa hali ya usalama katika eneo la sahel ambako makundi mbalimbali yenye silaha yamekuwa yakifanya mashambulizi makali katika miaka ya hivi karibuni.

"Hatua hii itaimarisha azimio la nchi za Muungano wa Sahel kuhakikisha kuwa zinakabiliana na tatizo la ukosefu wa usalama pamoja," anaongeza Sa'adou.

Hata hivyo, Sa'adou anasema serikali ya kijeshi nchini Niger lazima ifanye kazi kwa bidii zaidi ili kuhakikisha usalama wa ustawi wa raia wake ili kuhalalisha uungwaji mkono wa wananchi unaoonekana kufurahia kwa maamuzi yake ya kukuza uhuru wa nchi.

TRT Afrika