Rwanda yatuma majeshi wapya Msumbiji kuimarisha usalama

Rwanda yatuma majeshi wapya Msumbiji kuimarisha usalama

Msumbiji inakumbana na mashambulizi ya kigaidi
Rwanda imetuma wanajeshi nchini Msumbiji / Picha:Rwanda Wizara ya Ulinzi

Rwanda imetuma kikosi kipya nchini Msumbiji kwa ajili ya kulinda amani nchjini humo. Wanajeshi hao wanapokezana na wenzao waliopo kikazi tayari Msumbiji.

Kikosi kinachoongozwa na Meja Jenerali Alexis Kagame kilichoondoka ni sehemu ya kikosi kikubwa cha misaada kinachojumuisha zaidi ya wanajeshi 2000 walioko katika jimbo la Cabo Delgado.

Julai 2021 serikali ya Rwanda, kwa ombi la Serikali ya Msumbiji iliamua kupeleka askari wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na Jeshi la Polisi la Rwanda (RNP) katika Jimbo la Cabo Delgado, Msumbiji, lililokuwa limeathiriwa na ugaidi na ukosefu wa usalama.

Serikali ya Msumbiji imekuwa ikishirikiana na Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika nchini Msumbiji kulinda amani dhidi ya mashambulizi ya kigaidia, Ujumbe huu pamoja na Rwanda ulipeleka zaidi ya wanajeshi 3,000 mwezi Julai 2021 kukabiliana na Al-Shabaab.

Kikosi cha Rwanda kinaunga mkono juhudi za mamlaka ya serikali ya Msumbiji kuimarisha amani kwa kuendesha operesheni za mapambano na usalama, pamoja na kuleta utulivu na mageuzi katika sekta ya usalama.

Umoja wa mataifa unasema takriban watu milioni mbili kaskazini mwa Msumbiji wanahitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu , 2023 Cabo Delgado, Nampula na Niassa kutokana na kuendelea kwa athari za vita, ghasia na ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

TRT Afrika