Marburg Ilitangazwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa Septemba 2024/ Picha: Wizara ya Afya Rwanda 

Rwanda imesema mlipuko wa virusi hatari vya Marburg nchini humo umekwisha, na hakuna maambukizi mapya kwa takriban wiki mbili.

Mlipuko wa Marburg ulitangazwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa Septemba 2024 na Rwanda ilianza kutoa chanjo dhidi ya Marburg mwezi Oktoba.

"Tangu wakati huo tumekuwa tukipambana na virusi hivi ili kuhakikisha kuwa vimedhibitiwa nchini Rwanda," Waziri wa Afya Sabin Nsanzimana aliwaambia waandishi wa Shirika la Umoja wa Afrika la Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika CDC.

"Nina furaha sana kuripoti leo kwamba imepita karibu wiki mbili bila maambukizi mapya na mwezi bila kifo kinachohusiana na ugonjwa wa Marburg," alisema.

"Virusi vya Marburg nchini Rwanda vimekwisha," aliongezea.

Wagonjwa kuruhusiwa kwenda nyumbani

"Wagonjwa wote wanaotibiwa virusi hivi wanaruhusiwa kuondoka ... tunapiga hatua nzuri sana."

Mkuu wa Afrika CDC barani Afrika Jean Kaseya alikuwa amesema mwezi Oktoba kwamba virusi hivyo vimedhibitiwa.

Pia alisema kuwa hakuna hatari ya virusi kuenea katika mipaka ya nchi isiyo na bandari.

Marburg huambukizwa kwa wanadamu kupitia popo na ni familia moja ya virusi kama Ebola.

Homa ya Marburg inayoambukiza mara nyingi huambatana na kutokwa na damu na kunyong'onyea kwa kiungo.

Lakini mlipuko wa ugonjwa huo nchini Rwanda ulishuhudia kiwango cha chini zaidi cha vifo vya chini ya asilimia 23, kulikuwa na vifo 15 kati ya wagonjwa 66 wa Marburg.

Waziri wa Afya alisema kuwa wataalamu wa afya wanaendelea kuwa chonjo na wanafanya uchunguzi zaidi wa virusi katika popo wa matunda.

TRT Afrika