Rwanda imeiambia Umoja wa Mataifa kuwa kusimamishwa kwa kesi ya Felicien Kabuga, ambae ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi, ni hatua "ya kusikitisha" na "pigo kwa waathiriwa na walionusurika".
Robert Kayinamura, Naibu Mwakilishi Mkuu wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa alisema Jumatano.
"Rwanda imesikitishwa na uamuzi wa kesi ya Kabuga," Kayinamura alisema, akiongeza kuwa kusimamishwa kwa muda usiojulikana kumeweka "mfano mbaya sana," Kayinamura alielezea mkutano huo wa Umoja wa Mataifa.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliijadili ripoti ya Mahakama ya Kimataifa ya Rufaa (IRMCT), ambayo iliamua mnamo mwezi Juni 2023 kwamba Kabuga, ambaye anatuhumiwa kwa ufadhili wa mauaji ya kimbari Rwanda, "hastahili kushtakiwa" kutokana na uzee na tatizo la afya ya akili.
"Sababu zilizotolewa za kusimamisha kesi ya Kabuga - kwamba hafai kutokana na umri wake - ni kisingizio cha kusikitisha na pigo kwa waathiriwa na walionusurika," Kayinamura aliongezea.
" Umri wake haupaswi kumuacha kukabili matokeo ya matendo yake. Haki haijui umri. Ana umri wa miaka 88 pekee,” Kayinamura alibainisha.
Kabuga anashtakiwa kwa mauaji ya halaiki, uchochezi wa moja kwa moja na kufanya mauaji ya halaiki hadharani, kufanya njama ya kutekeleza mauaji ya halaiki, na mateso kwa misingi ya kisiasa, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uliofanyika nchini Rwanda mwaka 1994.
Mauaji ya 1994
Kati ya tarehe 6 Aprili 1994 na 17 Julai 1994, mauaji ya halaiki dhidi ya kabila la Watutsi yalitokea nchini Rwanda wakati Wahutu wenye itikadi kali walipowauwa zaidi ya Watutsi 800,000 walio wachache na Wahutu wenye msimamo wa wastani ndani ya siku 100.
Kwa mujibu wa Hati ya Mashtaka ya Mahakamya Kimataifa ya Rufaa, Kabuga, ambae ni mwanzilishi wa kituo cha redio cha RTLM, aliiendesha na wengine kwa namna ambayo iliendeleza chuki na unyanyasaji dhidi ya Watutsi na wengine na kwamba walikubali kusambaza ujumbe dhidi ya Watutsi kwa lengo la kuwaondoa kabila la Watutsi nchini Rwanda.