Wakimbizi hawa ni wa asili ya Eritrea, Ethiopia, Sudan, na Sudan Kusini ambao walikuwa wakijaribu kuingia Ulaya lakini badala yake walikwama Libya/ Picha UNHCR Rwanda

Rwanda imepokea wakimbizi 91 kutoka Libya.

Wakimbizi hawa ni wa asili ya Eritrea, Ethiopia, Sudan, na Sudan Kusini ambao walikuwa wakijaribu kuingia Ulaya lakini badala yake walikwama Libya.

Rwanda imewapokea chini ya mpango wake na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

"Tangu 2019, watu 2150 wamehamishwa na zaidi ya watu 1500 wamepewa makazi mapya katika nchi za tatu," UNHCR imesema.

Hili ni kundi la 17 la waomba hifadhi ambao wamehamishwa kutoka Libya hadi Rwanda tangu 2019 chini ya mpango wa Dharura ya Usafiri wa Anga (ETM).

Kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama ndani na karibu na mji mkuu wa Libya wa Tripoli, tarehe 10 Septemba 2019, Umoja wa Afrika, Serikali ya Jamhuri ya Rwanda na UNHCR zilitia saini Mkataba wa Makubaliano ya kuanzisha Mfumo wa Usafiri wa Dharura (ETM) kwa ajili ya kuwahamisha wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka Libya.

Kulingana na Wizara ya Mambo ya Dharura ya Rwanda na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR watu 6,000 wamekuja Rwanda tangu wakati huo.

Kati ya hawa, 1,600 tayari wamehamishwa katika nchi za tatu za Uropa na Amerika Kaskazini.

Changamoto ya wakimbizi kutoka Uingereza

Mnamo Machi 21, Seneti ya Rwanda ilipiga kura ya kuidhinisha mkataba wa Ushirikiano wa Uingereza na Rwanda ambapo watu wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza watatumwa Rwanda ambako maombi yao yangeshughulikiwa.

Lakini bado mipango hii haijafaulu kwani imeenedelea kupata pingamizi kutoak kwa wabunge mahakama ya Uingereza.

Mpango wa kwanza ulikabiliwa na upinzani na changamoto za kisheria karibu mara moja, na kuishia katika Mahakama ya Juu ya Uingereza, ambayo mnamo Novemba 2023 iliamua kuwa ni kinyume cha sheria na kutilia shaka usalama wa Rwanda.

Kufuatia uamuzi huo, Uingereza na Rwanda zilitia saini mkataba mpya wa uhamiaji mwezi Disemba 2023. Serikali ya Uingereza iliwasilisha mswada bungeni, ambao Januari 2024 Bunge la Commons lilipitisha.

Lakini bado inapata pingamizi kutoka kwa wabunge wengine.

TRT Afrika