Rwanda imetia saini makubaliano na mashirika ya kimataifa kuongeza ufadhili katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Ushirikiano huo wa sekta ya umma na binafsi utakusanya zaidi ya dola bilioni 9.2 za ziada ili kuongeza juhudi zake kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa nchini Rwanda.
Rwanda imefanya makubaliano hayo na shirika la kimataifa la fedha IMF, benki ya uwekezaji ya Uropa, Shirika la maendeleo la Ufaransa (AFD), Cassa Depositi e Prestiti (CDP) na International Finance Corporation (IFC).
"Ushirikiano ambao tumetangaza leo unawakilisha mabadiliko katika utoaji wa fedha za hali ya hewa na ni ishara ya imani katika mkakati wa muda mrefu wa hatua ya Rwanda kujisaidia kukumbana na athari ya tabianchi," Waziri Mkuu wa Rwanda, Dk. Edouard Ngirente amesema.
"Hii ni hatua muhimu katika safari yetu ya kufikia dhamira yetu kitaifa ambayo inakadiriwa kuwa dola bilioni 11 kufikia 2030," ameongezea.
Msaada huo mpya unaendeleza ufadhili wa dola za Kimarekani milioni 319 unaofikiwa na Serikali ya Rwanda kupitia mpango wa uhimilivu na endelevu (RSF) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Fedha ambazo Rwanda itapokea itaongezea kwa dola milioni 319 za ufadhili ambazo serikali hiyo ilipata kupitia mpango wa Shirika IMF.
Rwanda ambayo imekumbwa na mafuriko hivi majuzi ilizindua mkakati wa ukuaji wa Kijani na kustahimili hali ya hewa inayopendekeza hatua ambazo Rwanda inaweza kuchukua ili kuhakikisha ustawi katika mabadiliko ya tabianchi.