Rwanda inadai kuwa DRC inaunga mkono kundi lenye silaha, FDLR, ambalo lilihusika katika mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994. / Picha: Reuters

Rwanda imekaribisha wito wa kufanyika kwa mkutano wa pamoja wa kikanda kuhusu mzozo unaoendelea nchini DR Congo.

Kundi la waasi la M23, ambalo Umoja wa Mataifa na mataifa kadhaa wanasema linaungwa mkono na Rwanda, limeweza kusonga kwa kiasi kikubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuuchukua mji mkuu wa Goma na kuapa kuelekea hadi mji mkuu.

Ongezeko la machafuko hivi punde katika eneo lenye utajiri wa madini ambalo limekumbwa na miongo kadhaa ya mapigano yanayohusisha makumi ya makundi yenye silaha, limetatiza bara huku jumuiya za kikanda zikifanya mikutano ya dharura juu ya mvutano huo unaoendelea.

Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Afrika Kusini inayojumuihsa mataifa 16 siku ya Ijumaa ilitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa kilele na Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi nane ili "kujadiliana kuhusu hali ya usalama nchini DRC."

'Suluhu la kisiasa'

Wizara ya mambo ya nje ya Rwanda ilisema "inakaribisha kufanyika kwa mkutano wa kilele uliopendekezwa", na kuongeza katika taarifa yake kuwa "imekuwa ikishiniki mara kwa mara suluhisho la kisiasa kwa mzozo unaoendelea."

Kikao cha dharura cha SADC hakikuhudhuriwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda - ambaye si mwanachama wa kambi hiyo - lakini kiongozi wa Kongo Felix Tshisekedi alikuwepo.

Hapo awali, Kagame alionekana kwenye kikao cha dharura cha EAC wakati rais wa DR Congo hakuhudhuria.

Mkutano wa SADC uliitishwa baada ya wanajeshi kutoka nchi mbili wanachama, Afrika Kusini na Malawi, kuuawa katika mapigano ya Goma.

Wanajeshi hao walikua sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha umoja huo, kinachojulikana kama SAMIDRC (Misheni ya Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo).

Katika taarifa ya Jumapili, wizara ya mambo ya nje ya Rwanda ilikosoa uwepo wa kikosi hicho nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikisema kwamba hakipaswi kuwapo kwa sababu kinaongeza matatizo ambayo tayari yamekuwepo.

Kagame aliwahi kutoa matamshi kama hayo hapo awali.

Wakati Rwanda haijawahi kukiri kuhusika kijeshi katika kuunga mkono kundi la M23 ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa Julai iliyopita ilisema ina takriban wanajeshi 4,000 mashariki mwa DR Congo, na kuishutumu Kigali udhibiti wa kundi hilo.

Rwanda inadai kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaunga mkono na kuwahifadhi FDLR, kundi lenye silaha lililoundwa na viongozi wa zamani wa Wahutu ambao waliwaua Watutsi wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994 Rwanda.

TRT Afrika