Maafisa wa TPDF na RDF wakijadiliana mbinu za kuimarisha usalama wa mipaka./Picha: Wizara ya Ulinzi Rwanda

Maafisa wa Jeshi daraja la 5 la Rwanda (RDF) na wenzao kutoka brigedi ya 202 ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (TPDF) wamekutana wilaya ya Karage nchini kubadilishana mbinu za kuimarisha ulinzi wa mipaka.

Mkutano huo wa 11, pia uliangazia namna ya kushirikiana katika kutatua uhalifu kati ya mataifa, kulingana na RDF.

Hali kadhalika, maafisa hao walipitia mafanikio ya awali ya uimarishaji ulinzi na usalama wa mipaka.

Mkutano huo wa 11, pia uliangazia namna ya kushirikiana katika kutatua uhalifu kati ya mataifa, kulingana na RDF./Picha: Wizara ya Ulinzi Rwanda

Maafisa hao pia waliangazia mbinu na njia mpya za kukabiliana na changamoto za kiusalama, kwa jamii zinazoishi mipakani.

Brigedia Jenerali Elias Kwiligwa, ambaye ni kamanda wa brigedi ya 202 kutoka TPDF, aligusia matukio chanya ya vikao vya kiusalama kama vilivyoasisiwa na marais wa nchi hizo mbili.

“Ushirikiano wetu umetuwezesha kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi zetu. Ni muhimu kuendelea kushughulikia changamoto za kiusalama kwenye maeneo ya mipaka yetu,” alinukuliwa Brigedia Jenerali Kwiligwa kupitia taarifa ya RDF.

Maafisa hao wakiwa katika kikao cha pamoja./Picha:Wizara ya Ulinzi Rwanda

Maafisa hao, pia walipata fursa ya kutembelea maeneo ya Kyerwa na Karagwe, ambazo ni wilaya za mpakani kati ya nchi hizo mbili.

TRT Afrika