Viongozi wa dini wamehimizwa kufanya ukaguzi wa hali joto au uchunguzi mwengine wa kiafya kwa watu wanaoingia katika maeneo ya ibada / Picha kutoka CEJP RWANDA

Serikali ya Rwanda imetoa miongozo kuhusu namna ya kuzuia na kudhibiti virusi vya Marburg katika nyumba za ibada.

Bodi ya Utawala ya Rwanda imesema viongozi wa dini sasa wanafaa kuchukua hatua za kuhakikisha wanazuia kuenea kwa maambukizi katika maeneo yote ya ibada ili kuwalinda waumini dhidi ya kuambukizwa virusi hivyo.

Kulingana na Wizara ya Afya, kufikia Oktoba 6, kulikuwa na wagonjwa 49 waliothibitishwa kuwa na maambukizi. Kati ya hao, 29 walikuwa wakipokea matibabu, na watu 12 wamefariki huku nane wakipona.

Maagizo Mapya

Viongozi wa dini wamehimizwa kufanya ukaguzi wa halijoto au uchunguzi mwengine wa kiafya kwa watu wanaoingia katika maeneo ya ibada ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Marburg.

Pia wameombwa kuwahamasisha waumini wao kuchukua tahadhari, kufuata miongozo ya afya, kuepuka tabia hatarishi dhidi ya virusi vya Marburg.

Katika nyumba za ibada watu wanahimizwa kutofanya mawasiliano ya karibu na watu wanaoonyesha dalili za virusi vya Marburg au mtu yeyote anayeshukiwa kuambukizwa.

Makanisa na misikiti yameombwa kuepuka kuwapa watu sacramenti au kufanya desturi zozote zinazofanana na hizo ambazo zinaweza kuongeza kuenea kwa virusi vya Marburg.

Matambiko ya kuwaaga watu waliofariki yamepigwa marufuku ndani ya maeneo ya ibada kama ilivypo kawaida. Watu pia wamekatazwa kukaribia au kuandaa mwili wa mtu yeyote ambaye amekufa kutokana Marburg.

TRT Afrika