Rwanda 'inajua' uamuzi wa Uingereza kusitisha mpango wa wahamiaji

Rwanda 'inajua' uamuzi wa Uingereza kusitisha mpango wa wahamiaji

Rwanda inasema inafahamu nia ya Uingereza kusitisha makubaliano ya kuwatimua wahamiaji.
Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Keir Starmer anasema mpango wa kufukuzwa Rwanda "umekufa na kuzikwa." / Picha: AFP

Rwanda ilisema Jumatatu kwamba "inazingatia" uamuzi wa serikali mpya ya Leba nchini Uingereza kufuta makubaliano yenye utata ya kuwafukuza wanaotafuta hifadhi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Waziri Mkuu Keir Starmer alikuwa ametangaza Jumamosi kwamba mpango wa wahamiaji, uliobuniwa na serikali iliyotimuliwa ya Conservative, "ulikufa na kuzikwa."

Tayari kulikuwa na msururu wa changamoto za kisheria kwa mpango huo, ambapo Mahakama ya Juu ya Uingereza mnamo Novemba mwaka jana ilitoa uamuzi kwamba ulikuwa kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa.

"Rwanda inazingatia nia ya Serikali ya Uingereza kusitisha Mkataba wa Ushirikiano wa Uhamiaji na Maendeleo ya Kiuchumi, kama ilivyoainishwa chini ya masharti ya Mkataba uliopitishwa na mabunge yetu yote mawili," ofisi ya msemaji wa serikali Yolande Makolo ilisema katika taarifa yake.

'Tatizo la Uingereza'

"Ushirikiano huu ulianzishwa na Serikali ya Uingereza ili kushughulikia mgogoro wa uhamiaji usio wa kawaida unaoathiri Uingereza - tatizo la Uingereza, sio Rwanda," ilisema taarifa hiyo.

"Rwanda imeunga mkono kikamilifu upande wake wa makubaliano, ikiwa ni pamoja na kuhusu fedha, na inasalia kujitolea kutafuta suluhu la mzozo wa wahamiaji duniani, ikiwa ni pamoja na kutoa usalama, utu na fursa kwa wakimbizi na wahamiaji wanaokuja nchini mwetu."

Chama cha Labour Party kilisema kabla ya uchaguzi wa Julai 4 kwamba kitaachana na mpango huo, ambao serikali ya Conservative ilisema ulibuniwa kuzuia idadi kubwa ya wahamiaji wanaojaribu kuvuka mlango wa bahari wa English channel ya Ufaransa hadi Uingereza kwa boti kutoka kaskazini mwa Ufaransa.

Mapema mwaka huu, aliyekuwa Waziri Mkuu Rishi Sunak alikuwa amepitisha sheria bungeni inayoiona Rwanda kama nchi salama, kuruhusu safari za ndege za wahamiaji kuendelea licha ya wasiwasi kuhusu sheria za haki za binadamu.

Suala la kisiasa

Uhamiaji limekuwa suala kuu la kisiasa tangu Uingereza ilipoondoka kwenye Umoja wa Ulaya mwaka 2020, hasa kutokana na ahadi ya "kuchukua tena udhibiti" wa mipaka ya nchi.

Rwanda, ambayo ni makazi ya watu milioni 13 katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika, inadai kuwa mojawapo ya nchi tulivu zaidi barani humo na imejizolea sifa kwa miundombinu yake ya kisasa.

Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanamshutumu Rais mkongwe Paul Kagame kwa kutawala katika mazingira ya hofu, kukandamiza upinzani na uhuru wa kujieleza.

TRT Afrika