Serikali ya Rwanda leo imetangaza kuumalizika rasmi ugonjwa wa Marburg nchini humo.
Tamko hili linakuja baada ya siku 42 mfululizo bila maambukizi mapya kufuatia kuruhusiwa kwa mgonjwa wa mwisho kuondoka hospitalini, kulingana na miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Hii ni hatua muhimu kwa mfumo wa afya ya umma wa Rwanda. Wakati tunaomboleza maisha yaliyopotea, tunatiwa moyo na maendeleo yaliyopatikana," Waziri wa afya Rwanda Dkt. Sabin Nsanzimana amesema katika taarifa yake.
WHO imesema Rwanda imefikia kiwango cha kuwa salama dhidi ya Marburg.
"Mlipuko huo, uliothibitishwa tarehe Septemba 27, 2024, ulikuwa mlipuko wa kwanza wa Ugonjwa wa Virusi vya Marburg nchini Rwanda. Jumla ya maambukizi 66 yalithibitishwa na vifo 15 vilirekodiwa," WHO imesema katika taarifa.
"Uwezo wa Rwanda kukumbana na Marburg unaonyesha jinsi uongozi wa kujitolea, juhudi za pamoja za washirika na mfumo dhabiti wa afya ni muhimu katika kushughulikia dharura za afya ya umma, kuokoa na kulinda maisha na pia kulinda afya ya watu binafsi na jamii," alisema Dkt. Brian Chirombo, Mwakilishi wa WHO nchini Rwanda.
Takriban asilimia 80 ya maambukizi yalikuwa miongoni mwa wahudumu wa afya walioambukizwa walipokuwa wakitoa huduma kwa wenzao na wagonjwa wengine.
"Tumefikia hatua hii kwa sababu ya kujitolea kwa wahudumu wetu wa afya, serikali na washirika wetu ambao ushirikiano wao na hatua za haraka, zilizoratibiwa zilifanya iwezekane kudhibiti mlipuko huo kikamilifu," Dkt. Nsazimana aliongezea.
Tumefaulu kutambua asili ya virusi vya Marburg na tunaendelea kuimarisha mifumo yetu ya uchunguzi.