Ummy Mwlaimu ameondolewa kwenye nafasi ya Waziri wa Afya./Picha: X

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya uongozi ikiwemo Baraza la Mawaziri, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Taasisi.

Katika mabadiliko hayo, wakongwe wawili walioachwa hapo awali wamerudishwa.

Huyu sio mwengine bali ni Profesa Palamagamba Kabudi, mmbobezi wa sheria, ataiongoza Wizara ya Sheria na Katiba.

Naye William Lukuvi ameteuliwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.

Mabadiliko haya pia yameigusa Wizara nyeti ya Afya ambapo hivi sasa itakuwa chini ya Jenista Mhagama ambae kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.

Wizara ya Afya ilikuwa chini ya Ummy Mwalimu, ambae ameiongoza Wizara hiyo kwa miaka mingi, na kwa sasa amewekwa kando.

Wakati huo huo, Rais Samia amemteuwa Dkt Irene Isaka kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

Inaaminika kwamba, mabadiliko haya yaliyofanywa katika Wizara ya Afya, huenda yakawa yamechangiwa na sakata lililokuwa likiendelea kati ya Mfuko wa Bima ya Afya, na watoa huduma ya afya yaani hospitali.

Wizara ya Maliasili na Utalii imerudi kwa Pindi Chana, ambaye miaka miwili iliyopita, aliingoza Wizara hiyo hiyo.

Wizara ambazo kila kunapofanyika mabadiliko zinaonekana kuguswa ni ile ya Utalii, pamoja na Sheria na Katiba.

Je, hii inaashiria nini?

TRT Afrika