Kikosi cha dharura cha RSF nchini Sudan kimekaribisha wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kuwapa fursa ya kustahimili mzozo huo uliodumu kwa miezi 11.
Katika taarifa yake, RSF ilionyesha matumaini kwamba azimio la Baraza la Usalama "litapunguza kwa kiasi kikubwa mateso ya watu wa Sudan kwa kuhakikisha uwasilishaji mzuri wa misaada ya kibinadamu" na kuweka njia ya mchakato wa kisiasa utakaosababisha usitishaji vita wa kudumu.
Siku ya Ijumaa Baraza la Usalama lilipitisha azimio lililoandaliwa na Uingereza la kusitisha mapigano katika mwezi wa Ramadhani, lakini utaratibu wa kutekeleza azimio hilo bado hauko wazi.
Nia njema lakini hakuna utaratibu
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Al-Harith Idriss Al-Harith Mohamed, aliliambia baraza hilo siku ya Alhamisi kwamba rais wa baraza la mpito la nchi hiyo alipongeza wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa ajili ya kusitisha mapigano ndani ya mwezi wa Ramadhani. Hata hivyo, alisema kiongozi huyo "anashangaa jinsi ya hilo litatekelezeka."
"Katika kukumbatia pendekezo la usitishaji mapigano wa kibinadamu, tunaeleza utayari wetu wa kushiriki katika mijadala kuhusu uanzishwaji wa taratibu za ufuatiliaji zilizokubaliwa," RSF ilisema katika taarifa yake ya Jumamosi.
Ramadhani inatarajiwa kuanza Jumapili jioni.
Diplomasia ya Marekani
Kwa upande wake mjumbe maalum wa Marekani nchini Sudan, Tom Perriello, atazuru mataifa kadhaa barani Afrika na Mashariki ya Kati kuanzia Machi 11 hadi 25, Wizara ya Mambo ya Nje ilisema Jumamosi.
Ziara hiyo inanuiwa kuonyesha "kipaumbele ambacho Utawala unaweka katika kumaliza mzozo wa Sudan, kukidhi mahitaji ya haraka ya kibinadamu ya watu wa Sudan, na kupanga njia kuelekea serikali ya kiraia, ya kidemokrasia."
Perriello atazuru Uganda, Ethiopia, Djibouti, Kenya, Misri, Saudi Arabia, na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Vita vilizuka nchini Sudan Ramadhani ya mwaka jana, Aprili 15, 2023, kati ya jeshi la Sudan na RSF. Umoja wa Mataifa unasema karibu watu milioni 25 - nusu ya wakazi wa Sudan - wanahitaji msaada, wengine milioni 8 wamekimbia makazi yao na njaa inaongezeka. Washington inasema pande zinazohusika katika mzozo huo zimefanya uhalifu wa kivita.