Rais Samia alikuwa mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa Kimataifa ambao umewaleta pamoja viongozi kutoka sehemu mbalimbali. / Picha: Ikulu Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amekuwa mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa Kimataifa ambao umewaleta pamoja viongozi kutoka sehemu mbalimbali.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na washirika wa maendeleo wanaotarajiwa kuahidi dola bilioni 4 zinazohitajika kuwezesha kupatikana kwa nishati safi ya kupikia kwa wanawake milioni 250 wa Kiafrika ifikapo 2030.

Rais Samia alisema katika hotuba yake, "Licha ya Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu na rasilimali zote muhimu, ni bara la chini kuwa na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia".

Rais Samia amesema Afrika ni bara la chini kuwa na upatikanaji  wa nishati safi. / Picha: Ikulu Tanzania

Aliongeza kusema kuwa, "Zaidi ya Waafrika milioni 900 wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia, jambo ambalo linachangia uharibifu wa mazingira, upotevu wa bioanuai na athari za kiafya.

Aidha alitaja maeneo matatu muhimu ya nishati safi.

La kwanza hasa maeneo ya vijijini ni uwezo mdogo kutokana na gharama kubwa na upatikanaji wake pia ni tabu.

La pili ni ulimwengu kwa jumla kutolipa suala hilo kipaumbele. Ufadhili mdogo na watu kutokujua fursa za kiuchumi zilizopo kwenye nishati safi ya kupikia inayorejesha nyuma harakati hizo.

Rais Samia ametaja mambo matatu muhimu kuhusu nishati safi. / Picha: Ikulu Tanzania

Na pia kutokuwepo ushirikiano wa kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa wote. Rais Samia amesistiza upatikanaji, gharama ndogo na suluhu zinazotekelezeka.

Rais Samia pia amesisitza kuongezeka kwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia itachangia wanawake kupata fursa zaidi kushiriki shughuli nyingine za kiuchumi, kupunguza umaskini na usawa wa kijinsia.

La mwisho Rais alisema licha ya changamoto hizo, Tanzania ina dhamira ya kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa hivi karibuni uliokusudia kufikia 80% ya Watanzania wanaotumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.

Kulingana na Benki ya Maendelo ya Afrika, tukio hilo la kihistoria linalenga kuleta mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa Waafrika karibu bilioni moja wanaotumia nishati chafu, ambayo husababisha vifo vya mapema vya takriban nusu milioni ya wanawake na watoto kila mwaka.

TRT Afrika