Akihutubia kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, rais wa Malawi Lazarus Chakwera alisema nchi za Afrika zinapitia "magumu" katika kutimiza wajibu wao wa kulipa madeni.
"Tunajaribu kila linalowezekana kudhibiti madeni yetu, lakini kama unaweza kufikiria kurekebisha au kufuta kabisa baadhi ya madeni haya, Afrika itakuwa na 'nafasi ya kupumua," Chakwera alipendekeza.
Kulingana na Benki ya Dunia, deni la nje la Afrika liliongezeka kutoka $1.12 trilioni mwaka 2022 hadi $1.152 trilioni kufikia mwisho wa 2023.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Akinwuni Adesina hivi majuzi alionya katika mkutano wa UN mjini Washington kwamba mikopo "isiyo na uwazi" inayoungwa mkono na rasilimali inadhoofisha uwezo mkubwa wa kiuchumi wa Afrika, utatatiza utatuzi wa madeni na kuhatarisha ukuaji wa nchi kwa siku zijazo.
Kulingana na Adesina, nchi za Afrika zinatumia asilimia 65 ya Pato lao la Taifa katika kulipia deni la nje.
"Nadhani ni wakati wa sisi kuwa na uwazi wa madeni na uwajibikaji na kuhakikisha kuwa jambo hili lote la mikopo hii isiyo wazi inayofadhiliwa na maliasili inaisha, kwa sababu inatatiza suala la deni na suala la utatuzi," aliongeza.
Hivi karibuni, Benki ya Dunia na serikali ya Marekani wameitaka Malawi "kusimamia ipasavyo" deni lake la nje, ambalo kwa sasa lina jumla ya dola bilioni 4.