Sudan imeomba mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kile inachokiita UAE "uchokozi" kwa madai ya kusaidia wanamgambo wanaopambana na jeshi, chanzo cha kidiplomasia kilisema Jumamosi.
Mapigano yalizuka mwezi Aprili mwaka jana kati ya jeshi la kawaida, linaloongozwa na kiongozi mkuu wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan, na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kinachoongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo.
Kwa miezi kadhaa, jeshi la kawaida limeshutumu Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuunga mkono RSF, madai ambayo UAE inakanusha.
"Jana, mwakilishi wetu wa kudumu katika Umoja wa Mataifa aliwasilisha ombi la kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kujadili uchokozi wa UAE dhidi ya watu wa Sudan, na utoaji wa silaha na vifaa kwa wanamgambo wa kigaidi," chanzo kiliiambia AFP.
UAE inakanusha madai
Shirika rasmi la habari la nchi hiyo SUNA limethibitisha kuwa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa Sudan, Al-Harith Idriss, ndiye aliyewasilisha ombi hilo.
SUNA ilimnukuu Idriss akisema hii ilikuwa "kujibu risala ya mwakilishi wa UAE kwa Baraza", na kwamba "uungaji mkono wa UAE kwa wanamgambo wa Msaada wa Haraka walioendesha vita dhidi ya serikali unaifanya UAE kuwa mshirika katika uhalifu wake wote".
Katika barua kwa Baraza la Usalama wiki iliyopita, wizara ya mambo ya nje ya UAE ilikataa shutuma za Sudan kwamba inaunga mkono RSF.
Barua hiyo ilisema madai hayo "ni ya uwongo (na) hayana msingi, na hayana ushahidi wowote wa kuaminika wa kuyaunga mkono".
'Wasiwasi mkubwa'
Kando siku ya Jumamosi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilionyesha "wasiwasi mkubwa" juu ya kuongezeka kwa mapigano katika jimbo la Kaskazini la Darfur nchini Sudan na kuonya dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya karibu ya RSF na wanamgambo washirika dhidi ya El Fasher.
Mji huo ndio mji mkuu wa mwisho wa jimbo la Darfur ambao hauko chini ya udhibiti wa RSF na unahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa walitoa onyo kama hilo Ijumaa, huku Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Turk akielezea "wasiwasi wake mkubwa."
Ofisi ya msemaji wa Katibu Mkuu Antonio Guterres ilisema shambulio dhidi ya El Fasher "litakuwa na matokeo mabaya kwa raia ... katika eneo ambalo tayari liko kwenye ukingo wa njaa."
Maelfu waliuawa
Vita vya Sudan vimeua maelfu ya watu na kuwalazimu zaidi ya watu milioni 8.5 kuyakimbia makazi yao katika kile ambacho Umoja wa Mataifa umekiita "mgogoro mkubwa zaidi wa watu kuhama makwao duniani."
Mwezi Disemba, Khartoum iliwataka wanadiplomasia 15 wa Imarati kuondoka nchini humo baada ya kamanda wa jeshi kumshutumu Abu Dhabi kwa kuunga mkono RSF, na maandamano huko Port Sudan yalidai kufukuzwa kwa balozi wa UAE.