Rais wa Comoro Azali Assoumani, ambaye aliingia madarakani mwaka 1999 kupitia mapinduzi na kushinda chaguzi nne katika taifa hilo la visiwa vya Bahari ya Hindi tangu mwaka 2002, amekanusha kuwa ana nia ya kukabidhi madaraka kwa mwanawe.
Ushindi wa hivi punde zaidi wa Assoumani ulikuja mnamo 2024, ingawa matokeo yalikataliwa na upinzani ambao ulisema kuwa kura hiyo iligubikwa na dosari.
Rais alisema Alhamisi katika hotuba yake kwa wafuasi wake katika kisiwa cha Moheli: "Nitamweka mwanangu kuchukua nafasi yangu kama mkuu wa serikali na chama."
Walakini, katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa Facebook mwishoni mwa Ijumaa, afisi ya rais ilisema hiyo haimaanishi kuwa alikusudia kukabidhi mamlaka atakapoondoka madarakani 2029 kwa mwanawe Nour El Fath.
"Serikali inapenda kusisitiza kwamba hakuna wakati Rais Azali alizungumza juu ya uwezekano wa kurithi wa mwanawe Nour El Fath, kama mkuu wa nchi," ilisema.
'Urithi wa familia'
"Badala yake alizungumzia 'mtoto' ambaye angemrithi, akijua kwamba ni desturi katika Comoro kuelezea kila raia kama 'mtoto', bila kutaja kizazi cha mtu mwenyewe."
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa rais hapo awali alikataa wazo la "urithi wa familia" na kwamba mrithi wake angetoka Anjouan, mojawapo ya Visiwa vitatu vikuu vya Comoro.
Kulingana na katiba ya Comoro, urais lazima uzunguke kati ya Visiwa vitatu kila baada ya miaka 10.
El Fath kwa hivyo hatastahili kuchukua nafasi ya babake mwishoni mwa muhula wa urais mwaka wa 2029 isipokuwa katiba itabadilishwa.
Mamlaka ya baraza la mawaziri
Rais amemweka mwanawe msimamizi wa kuratibu masuala ya serikali na kumpa mamlaka makubwa juu ya baraza la mawaziri.
Chama chake tawala kilishinda uchaguzi wa bunge mwezi huu, ingawa vyama vya upinzani vilisusia kura hiyo au kukataa matokeo kwa madai kuwa kulikuwa na udanganyifu.
Comoro ina wakazi wapatao 800,000. Imeshuhudia takriban mapinduzi 20 au majaribio ya mapinduzi tangu ilipojinyakulia uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1975.