Azali Assoumani amewahi kuwa Rais wa Comoro kwa vipindi kadhaa. / Picha: Reuters

Mwanamume aliyemshambulia Rais wa Comoro Azali Assoumani kwa kisu na kumjeruhi kidogo amepatikana amefariki gerezani, mwendesha mashtaka wa kitaifa alisema Jumamosi, siku moja baada ya tukio hilo.

"Alitengwa katika seli ili atulie jana baada ya kukamatwa. Wachunguzi walikuta mwili wake usio na uhai ukiwa umelala sakafuni asubuhi ya leo. Daktari alitangaza kuwa amefariki," Ali Mohamed Djounaid aliambia mkutano na waandishi wa habari.

"Uchunguzi umeanzishwa ili kubaini chanzo cha kifo chake," aliongeza.

Msemaji wa serikali Fatima Ahamada alisema Jumamosi kwamba Assoumani mwenye umri wa miaka 65 alikuwa nyumbani na familia yake na "anaendelea vizuri sana".

Shambulio hilo lilitokea wakati wa mazishi ya kiongozi mashuhuri wa kidini.

Kisu hicho kilijeruhi mkono wa rais, lakini mshambuliaji alizuiwa na muombolezaji mwingine, walioshuhudia walisema.

TRT Afrika