Hakuna sababu iliyotolewa ya kufutwa kazi kwa Audace Niyonzima. / Picha: Reuters

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amemfuta kazi Waziri wake wa Fedha Audace Niyonzima Jumatatu, siku chache baada ya Shirika la Kodi nchini humo kuripoti upungufu wa mapato katika kipindi cha miezi minne iliyopita.

Ndayishimiye alimtaja Nestor Ntahontuye kuwa Waziri mpya wa Fedha akichukua nafasi ya Audace Niyonzima.

Ingawa hakuna sababu zilizotolewa, kufukuzwa kwa Niyonzima kumekuja siku chache baada ya mamlaka ya mapato ya Burundi kuripoti kuwa imeshindwa kufikia malengo ya mapato kwa zaidi ya faranga za Burundi bilioni 110 (dola milioni 37) huku kukiwa na uhaba wa mafuta na fedha za kigeni nchini humo.

Awali Niyonzima alitahadharisha kuwa ikiwa haitabadilishwa, nakisi hiyo inaweza kuathiri uwezo wa Serikali wa kutekeleza bajeti yake ya kila mwaka. Hadi hivi majuzi Ntahontuye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha katika Bunge la Kitaifa la Burundi.

Waziri huyo mpya ana shahada ya uhandisi wa takwimu, akibobea katika ufuatiliaji na tathmini ya miradi.

Awali alikuwa na jukumu la kupanga, ufuatiliaji na tathmini katika mashirika mbalimbali nchini. Uchumi wa Burundi unategemea sana kilimo, hasa uzalishaji wa chai na kahawa.

TRT Afrika