Alain Guillaume Bunyoni waziri mkuu wa zamani wa Burundi ameiomba mahakama kumuacha kutokana na sababu za kiafya/ Picha: Wengine 

Waendesha mashtaka nchini Burundi wametaka waziri Mkuu wa zamani Alain-Guillaume Bunyoni ahukumiwe kifungo cha maisha kwa tuhuma kadhaa ikiwemo za kutishia maisha ya rais.

Hii ni kwa mujibu wa chanzo cha mahakama na mashahidi.

Bunyoni amekuwa akishikiliwa tangu mwezi Aprili na kufikishwa mahakama kuu mwezi Septemba katika gereza lililopo katika mji mkuu wa kisiasa wa Gitega.

Bunyoni alikuwa waziri mkuu kuanzia katikati ya mwaka 2020 hadi Septemba 2022 alipotolewa katika nafasi hiyo, siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuonya kuhusu njama ya "mapinduzi" dhidi yake.

Bunyoni ambaye alipandishwa kizimbani siku ya Alhamisi akiwa na washtakiwa wenzake sita, amekana mashitaka yanayomkabili na kusema aachiwe huru kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi.

'Jaribio la kupindua serikali'

Jenerali huyo wa jeshi anatuhumiwa kutumia mbinu za kishirikina kutishia maisha ya mkuu wa nchi, kudhoofisha usalama wa taifa, kujaribu kuangusha taasisi za serikali, kuyumbisha uchumi na kujitajirisha kinyume cha sheria, miongoni mwa mashtaka mengine.

Alain-Guillaume Bunyoni anashitakiwa kwa tuhuma kadhaa ikiwemo za kutishia maisha ya rais Evariste Ndayishimiye/ Picha Reuters 

"Kwa sababu hizi zote, naomba Alain-Guillaume Bunyoni aadhibiwe kwa kifungo cha maisha," mwendesha mashtaka Jean-Bos co Bucumi alisema.

Pia alimtaka alipe faini ya faranga za Burundi milioni 7.1 (karibu dola 2,500) na "ambayo ni sawa na mara mbili ya thamani ya nyumba 153 na viwanja na magari 43 zake."

Upande wa mashtaka pia uliomba kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya wengine sita waliopandishwa kizimbani, wakiwemo washitakiwa wenza wawili wakuu, kanali wa polisi na wakala mkuu wa upelelezi.

Jaji kiongozi alisema hukumu itatolewa ndani ya siku 30.

Mkuu huyo wa zamani wa polisi na waziri wa usalama wa ndani, Bunyoni alionekana kama mkuu wa baraza la viongozi wa kijeshi wanaojulikana kama "majenerali" ambao walikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini Burundi.

Mshirika wa karibu wa rais wa zamani Pierre Nkurunziza, Bunyoni alikuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha CNDD-FDD.

TRT Afrika