Rais wa Jamhuri ya Tanzania Samia Suluhu Hassan amemfuta kazi Nape Nnauye kama waziri wa habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na badala yake kumtangaza Jerry William Slaa kuchukua wadhifa huo.
Kabla ya uteuzi huo, Slaa alikuwa akihudumu kama waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi.
Nape ambaye ndiye mbunge wa jimbo la Mtama mkoani Lindi, ameshika wadhifa huo wa waziri wa habari tangu mwaka 2022.
Ni mzoefu wa Diplomasia na Mahusiano ya Kigeni na Sayansi ya Jamii ambapo anashikilia shahada kutoka Kituo cha Mahusiano ya Nje na Chuo cha Sayansi ya Jamii cha Kivukoni, mtawalia. Kwa sasa, ni mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya Sheria (LLB) katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Rais pia amempandisha cheo Ridhiwani Jakaya Kikwete kuwa waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, VIjana, Ajira na wenye ulemavu). Kabla ya uteuzi huu, Kikwete alikuwa naibu waziri, ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa umma na Utawala bora
January Makamba pia ameondolewa kama waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye nafasi yake sasa itakchukuliwa na aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia Mahmoud Thabit Kombo.
Rais Samia hakutangaza Makamba atahamishwa kitengo kipi japo kumekuwa na mjadala mtandaoni wa uwezekano kuteuliwa kuwania Uenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika AU.
Iwapo kweli Makamba atawania Uenyekiti huo, basi atakuwa anjiunga katika kinyang'anyiro hicho na wagombea wengine kutoka Kenya na Djibouti.
Hii pia itaonekana kama kinyume na tangazo la hapo awali mwezi Machi, ambapo Rais wa Kenya William Ruto alitangaza kuwa Afrika Mashariki imekubaliana kumuunga mkono Mgombea mmoja kwa nafasi hiyo.
Rais Ruto alikuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa awali wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.
“Kwa mtazamo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumeshauriana kama wakuu wa nchi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, na tumekubali kudhamini mgombea mmoja kama wana Afrika Mashariki,'' Rais Ruto alisema.
Deogratius John Ndejembi amehamishwa kuwa waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Tangazo hilo la Rais pia lilijumuisha uteuzi wa Manaibu Waziri na Makatibu wa mikoa.