Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amesema Senegal ni nchi huru, na uhuru haukubali uwepo wa kambi za kijeshi za kigeni katika nchi huru / Picha: Reuters 

Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye asema Ufaransa inapaswa kufunga kambi zake za kijeshi katika taifa hilo la Afrika Magharibi wakati ikijiandaa kuadhimisha miaka 80 ya mauaji ya kikoloni.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikiri kwamba wanajeshi wa nchi yake walihusika na "mauaji" ya wanajeshi wa Senegal mnamo 1944, Faye aliliambia Shirika la Habari la AFP siku ya Alhamisi.

Faye alipongeza uthibitisho huo lakini akasema kuwa kuruhusu vituo vya Ufaransa nchini hakuendani na uhuru wa kitaifa.

"Senegal ni nchi huru, na uhuru haukubali uwepo wa kambi za kijeshi za kigeni katika nchi huru," Faye alisema katika mahojiano katika ikulu ya rais.

Kufukuza vikosi vya Ufaransa

Faye aliingia madarakani katika uchaguzi wa Machi akiahidi kukomesha utegemezi kwa mataifa ya kigeni.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa hiyo haimaanishi kukata uhusiano kabisa na Ufaransa.

Nchi nyingine kadhaa zinazozungumza lugha ya kifaransa katika magharibi na kati mwa Afrika, zikiwemo Mali, Burkina Faso na Niger, ambazo zinaongozwa na viongozi kijeshi, wamevifukuza vikosi vya Ufaransa na kugeukia washirika mbadala kwa ajili ya msaada wa ulinzi.

Ripoti zinaonyesha Ufaransa ina mpongo wa kupunguza wanajeshi wake Afrika, kutoka wanajeshi 350 hadi 100 nchini Senegal na Gabon na hadi 300 nchini Chad kutoka 1,000. Pia wanapanga kupunguza kutoka wanajeshi 600 hadi 100 nchini Côte d'Ivoire.

"Ufaransa inasalia kuwa mshirika muhimu wa Senegal kwa uwekezaji na uwepo wa makampuni ya Ufaransa na hata raia wa Ufaransa ambao wako Senegal," Rais Faye alisema.

Macron akiri mauaji

Rais wa Senegal alisema alipokea barua kutoka kwa Rais wa Ufaransa Macron akikiri kosa la Ufaransa kwa mauaji ya wakati wa Vita vya Pili vya Dunia huko Thiaroye mnamo Desemba 1, 1944.

Ukatili huo kwa muda mrefu umekuwa mzozo kati ya Paris na Dakar.

Mnamo Novemba 1944, karibu wanajeshi 1,600 wa Kiafrika ambao walipigania Ufaransa na kufanywa wafungwa wa vita na Ujerumani, walirudishwa Dakar, kulingana na mwanahistoria wa Ufaransa Armelle Mabon.

Mara baada ya kuwasili katika kambi ya Thiaroye, nje kidogo ya Dakar, walipinga kucheleweshwa kwa mishahara, huku wengine wakikataa kurejea katika nchi zao bila malipo.

Vikosi vya Ufaransa viliwafyatulia risasi waandamanaji, na kuwauwa takriban 35, ingawa wanahistoria wanasema idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi.

TRT Afrika