Rais Azali Assoumani wa Comoro./Picha: Getty

Rais wa Comoro Azali Assoumani "anaendelea vyema" licha ya kushambuliwa kwa kisu siku ya Ijumaa na askari polisi ambaye baadaye alipatikana amekufa, maofisa nchini humo wamesema.

"Rais anaendelea vizuri. Hana tatizo lolote la kiafya. Alishonwa nyuzi kadhaa," alisema Waziri wa Nishati wa nchi hiyo Aboubacar Saïd Anli katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumamosi.

Azali alishambuliwa na kujeruhiwa wakati akihudhuria ibada ya mazishi, kulingana na ofisi ya rais wa nchi hiyo. Sababu ya shambulio hiyo bado haijajulikana.

Ahmed Abdou, mtu anayeaminika kuhusika na kutekeleza shambulizi hilo alichukua mapumziko ya kazi siku ya Jumatano iliyopita, kabla ya kufanya shambulizi hilo siku ya Ijumaa.

"Abdou aliwekwa rumande kabla hajapatikana amekufa siku ya Jumamosi asubuhi," alisema Ali Mohamed Djounaid, mwendesha mashitaka nchini humo.

Kulingana na mwendesha mashitaka huyo, uchunguzi bado unaendelea kujua chanzo cha shambulio hilo na kifo cha Abdou.

Assoumani aliapishwa kama kiongozi wa nchi hiyo kwa muhula wake wa nne mwezi Mei mwaka huu, kufuatia uchaguzi uliofanyika mwezi Januari.

TRT Afrika