Watu tisa waliuawa na 10 kujeruhiwa katika shambulizi lililodumu kwa saa sita lililofanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab kwenye hoteli iliyo ufukweni mwa mji mkuu wa Somalia Mogadishu, polisi walisema Jumamosi.
Waliouawa ni pamoja na raia sita na askari watatu wa vikosi vya usalama wakati wa operesheni ya uokoaji. Zaidi ya hayo, Abdikadir Abdirahman, mkurugenzi wa huduma ya gari la wagonjwa la Aamin, alisema kundi lake lilikuwa limebeba watu 20 waliojeruhiwa kutoka eneo la tukio.
Washambuliaji hao walivamia hoteli ya Pearl Beach kabla ya saa mbili usiku siku ya Ijumaa (1700 GMT). Shambulio hilo lilimalizika mwendo wa saa nane usiku, polisi walisema, baada ya makabiliano makali ya risasi kati ya vikosi vya usalama na wanamgambo hao, ambao wote waliuawa wakati wa majibizano ya risasi.
"Vikosi vya usalama vilifanikiwa kuwaokoa watu 84 wakiwemo wanawake na watoto na wazee," taarifa ya polisi ilisema.
Eneo ambalo shambulizi limefanyika
Hoteli ya Pearl Beach iko chini ya barabara kutoka kwa Ubalozi wa Uturuki na ni maarufu kwa maafisa wa serikali.
Shahidi Hassan Abdirahman aliliambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba alikuwa katika mgahawa huo wakati huo. "Nilisikia milio ya risasi kutoka upande wa ufuo na kufuatiwa na sauti kubwa ya mlipuko." Alisema kuwa alitoroka na kuona magari yaliyoharibika kando ya barabara.
Shahidi mwingine Mulki Osman alisema yeye na marafiki zake "walikimbia papo hapo kujificha" katika mgahawa waliposikia milipuko na milio ya risasi muda mfupi kabla ya saa nane usiku [saa za ndani].
"Baadhi ya marafiki zangu bado wamekwama ndani ya hoteli, lakini maafisa wa usalama walifanikiwa kuniokoa. Natumai watakaa salama," alisema.
Ufukwe wa Lido ni mojawapo ya maeneo maarufu zaidi ya Mogadishu na huwa na shughuli nyingi siku za Ijumaa usiku huku Wasomali wakifurahia wikendi kwa kutembelea maduka ya kahawa na vibanda vya aiskrimu.
Muungano wa Al Qaeda Afrika Mashariki, Al Shabab, umedai kuhusika na shambulio hilo.
Kundi la kigaidi lenye makao yake nchini Somalia linajulikana kwa kufanya mashambulizi kwenye hoteli na maeneo mengine yenye hadhi ya juu mjini Mogadishu, kwa kawaida huanza na shambulio la kujitoa mhanga.