Raia wa Nigeria wakikimbia mapigano nchini Sudan 

Idadi kubwa ya Wanigeria wanaokimbia mapigano nchini Sudan wamekwama kwenye mpaka wa Misri kwa sababu ya masuala ya visa.

Serikali ya Nigeria ilikuwa imewahamisha raia wake kutoka Sudan na walikuwa wakisafiri kwa msafara wa mabasi kuvuka mpaka kabla ya kusafirishwa kwa ndege hadi nchini mwao.

Lakini mamlaka ya Nigeria inasema waliohamishwa ''hawaruhusiwi kuvuka mpaka na kuingia Misri tangu wawasili Alhamisi jioni.''

Mkuu wa Kamisheni ya Wanigeria katika Diaspora Abike Dabiri-Erewa alisema katika taarifa yake kwamba Wanigeria hao ni miongoni mwa wageni wapatao 7000 waliozuiliwa na mamlaka ya Misri ambao ''wanasisitiza kupata visa na Waafrika wenzao ili kurejea katika nchi zao.''

Ujumbe wa Nigeria nchini Misri ''umekuwa ukifanya kazi bila kuchoka katika hili'' Dabiri-Erewa aliongeza. Afisa huyo wa Nigeria alitoa wito kwa mamlaka ya Misri ''kuwaruhusu wasafiri ambao tayari wamepatwa na kiwewe kupita katika nchi zao za mwisho katika mataifa mbalimbali barani Afrika'' kwa kuweka ''hali ya kibinadamu''.

Hakukuwa na maoni ya haraka kutoka kwa mamlaka ya Misri juu ya hali hiyo.

Serikali ya Nigeria ilikuwa imetangaza siku ya Alhamisi kwamba karibu raia 2,000, wengi wao wakiwa wanafunzi, wamehamishwa kutoka Sudan na walikuwa wakielekea nchi jirani ya Misri kwa mabasi 13.

Kundi la kwanza lilipangwa kuwasili Ijumaa, kulingana na serikali ya shirikisho.

Maelfu wameikimbia Sudan tangu Jumatatu huku mapigano kati ya wanajeshi na wanamgambo wa Rapid Support Forces yakiongezeka.

Usitishaji mapigano umevunjwa mara kwa mara na vikosi vinavyopingana na juhudi za kuwaleta kwenye meza ya mazungumzo zimezaa maendeleo kidogo.

TRT Afrika