Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, David Misime./Picha: TRT Afrika

Jeshi la Polisi chini Tanzania limepiga marufuku maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Maandamano hayo ya Septemba 23, 2024 yalikuwa yameratibiwa kufanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Septemba 13, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, David Misime ametoa onyo kwa viongozi wa CHADEMA kuacha kuhamasisha wananchi kuacha kujihusisha katika uhalifu huo na kuongeza kuwa, yeyote atakayeingia barabarani, atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi.

"Kwa maana hiyo, maandamano hayo yamepigwa marufuku. Jeshi la Polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo, asithubutu kufanya hivyo kwani maandamano hayo ni haramu na hayatofanyika," alisema Misime.

Msemaji huyo, pia amewataka Watanzania wasipoteze muda na gharama zao kushiriki katika maandamano hayo, na kuwarai wananchi wapenda amani kutokubali kudanganywa, kurubuniwa au kushawishiwa kwa namna yoyote ile kushiriki kwenye maandamano hayo.

"Badala yake, ni vyema wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za viasharia vyoyote vya uvunjivu wa amani," alieleza.

Kulingana na Misime, CHADEMA inalenga kuliondoa Jeshi la Polisi Tanzania kwenye za kiupelelezi zinazoendelea baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuviagiza vyombo vya uchunguzi, kufanya uchunguzi na kisha kuwasilisha taarifa kwake.

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe./Picha: TRT Afrika

Rais Samia alitoa kauli hiyo kufuatia kutekwa na kuuwawa kwa aliyekuwa mjumbe wa Sekretariati ya CHADEMA, Ali Mohamed Kibao mapema mwezi Septemba.

Siku ya Septemba 11, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alitangaza maandamano hayo kuanzia Septemba 23, 2024, iwapo serikali ya Tanzania haitashughulikia madai ambayo wameyataka yatekelezwe na Serikali.

Moja ya madai hayo ni pamoja kuishinikiza serikali kuachilia watu waliotekwa.

TRT Afrika