Papua New Guinea imeuarifu Umoja wa Mataifa kuwa zaidi ya watu 2,000 walifukiwa na maporomoko makubwa ya ardhi, kulingana na nakala ya barua iliyoipata shirika la habari la AFP.
"Maporomoko hayo yamefukia zaidi ya watu 2,000 na kusababisha uharibu mkubwa," idara ya majanga ya nchi hiyo imeutaarifa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Port Moresby.
Kijiji cha Enga kiliathirika zaidi kufuatia kuporomoka kwa Mlima Mungalo mapema Ijumaa asubuhi, na kufukia watu wengi walipokuwa wamelala.
Maporomoko hayo yamesababisha "uharibifu mkubwa wa majengo na kuathiri uchumi wa nchi hiyo," ilisema idara hiyo.
Njia kuu ya kuelekea mgodi wa Porgera "ilizibwa kabisa,", ilisema taarifa hiyo kama ilivyopokelewa na maofisa wa Umoja wa Mataifa Jumatatu asubuhi.
"Hali bado haijatulia kwani maporomoko hayo yanazidi kusogea taratibu, na kusababisha hatari kwa manusura na waokoaji."
"Ukubwa wa tatizo hilo unahitaji hatua za haraka na kutoka kwa makundi mbalimbali," imesema idara ya majanga ya nchi hiyo.
Pia imeitaka Umoja wa Mataifa kuiarifu Papua New Guinea "washirika wa maendeleo" na "marafiki wengine" wa kimataifa kuhusu suala hilo.
Msaada unapaswa kuratibiwa kupitia kituo cha maafa, ilisema.
Picha za mitandao ya kijamii zilizotumwa na wanavijiji na timu za vyombo vya habari vya eneo hilo zilionesha watu wakichimba kwa majembe, fimbo na mikono yao wazi ili kupata manusura, huku vilio vya wanawake vikisikika.
Vyombo vya habari vya Papua New Guinea siku ya Jumatatu viliripoti kwamba wakazi walikuwa wamewaokoa wanandoa waliokuwa wamekwama chini ya vifusi baada ya kusikia kilio chao cha kuomba msaada.
Hali ya hatari
Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji lilisema kuwa maji yanayoendelea kutiririka chini ya vifusi hivyo kuwa hatari sana kwa wakazi na vikosi vya uokoaji.
Serhan Aktoprak, afisa mwandamizi wa Shirika hilo nchini humo, aliiambia televisheni ya ABC kuwa wataendelea na zoezi la uokoaji hadi hapo litakapositishwa.
Aktoprak alisema kuwa vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kuokoa magari nane huku wakiwa na matumaini ya kupokea vyanzo zaidi.
Takribani watu 1,250 wamekosa makazi kutokana na maporomoko hayo yaliyotokea katika jimbo la Enga, siku ya Ijumaa.
Zaidi ya nyumba 150 zilikuwa zimefunikwa na maporomoko hayo huku nyingine 250 zikiachwa bila wakazi.
"Nyumba hizo zilikuwa chini ya tope la mita nane. Tumekutana na taka nyingi na ngumu katika zoezi la uokoaji," alisema Justine McMahon, mkurugenzi mkazi wa CARE International. Takribani watu 4,000 wanaishi karibu na maeneo yaliyoathirka zaidi, amesema.
Nchi majirani za Australia na Ufaransa zimesema kuwa ziko tayari kutoa msaada wa Papua New Guinea.