Nini mustakabali wa raia 178,000 wa Zimbabwe walioko Afrika Kuisini?

Nini mustakabali wa raia 178,000 wa Zimbabwe walioko Afrika Kuisini?

Kati ya dola bilioni 1.66 fedha za kigeni zilizoingia nchini Zimbabwe 40% zilitokea Afrika Kusini.
Raia wa Zimbabwe  Siyayi Chinemhute, anayeishi kisheria nchini Afrika Kusini , anawasiwasi juu ya hatma yake na familia yake. Picha : Reuters

Patricia Marima, mama wa watoto wanne kutoka Zimbabwe aliyeishi katika mji wa Benoni karibu na Johannesburg Afrika Kusini tangu 2008, anahisi kupata utulivu kiasi, kwasababu ana hadi Desemba kuandaa makaratasi yake ili kuhalalisha kukaa kwake nchini humo.

Kama ilivyo kwa wengi kutoka nchi yake ya asili wenye makao yao nchini Afrika Kusini, Marima alihisi kutua mzigo baada ya waziri wa mambo ya ndani Pakishe Aaron Motsoaledi kutoa agizo la uhamiaji wiki iliyopita.

Agizo hili linatoa muda wa miezi sita wa msamaha kwa wastani wa wazimbabwe 178,000 wanaokabiliwa na kufukuzwa mwishoni mwa Juni isipokuwa kama waliomba vibali vya kuhalalisha kukaa kwao.

"Kuongezewa muda huu ni jambo ambalo sikutarajia, lilinishtua, sababu ni kwamba limeongezwa mara mbili hapo awali, na sasa kwa mara ya tatu," Patricia Marima anaiambia TRT Afrika.

''Nina matumaini kwamba makaratasi yetu yatakuwa tayari kufikia Desemba. Nataka kukaa hapa kwa ajili ya watoto wangu wanne, kwa maana maisha yao yako hapa," anasema.

Vibali ambavyo viliwaruhusu Wazimbabwe kuishi, kufanya kazi na kusoma nchini Afrika Kusini vilitarajiwa kuisha Juni 30, na kuwaacha wamiliki na chaguo la kuomba visa ya ziada au kurejea Zimbabwe.

Takriban Wazimbabwe 773,000 wana makazi nchini Afrika Kusini na kutafuta ajira, kulingana na takwimu za sensa ya mwaka 2022 kutoka Shirika la Takwimu la Taifa la Zimbabwe. Wenye Vibali vya kukaa nchini Zimbabwe (ZEP) ni takriban 178,000.

Mpango wa ZEP ulianza wakati seŕikali ya Afrika Kusini ilipotoa "uhusiano maalumu" kwa wazimbabwe ambao walikuwa nchini humo kinyume cha sheria, wengi wao wakiwa wamekimbia kukosekana kwa utulivu wa kiuchumi na kisiasa katika ardhi yao ya asili.

Raia wengi wa Zimbabwe walio na vibali aina ya ZEP waliwasili nchini Afrika Kusini zaidi ya muongo mmoja uliopita Picha: Reuters 

Seŕikali ya Afŕika Kusini ilibadilisha utoaji wa visa maalum kwa wazimbabwe waliokuwa na vibali maalum (ZSP) mwaka 2014, na tena mwaka 2017 na kuanzishwa kwa mfumo wa ZEP.

"Tumekuwa tukipokea kati ya maombi 1,000 - 1,500 kila siku," Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini linamnukuu waziri Motsoaledi akisema.

Makosa ya mara kwa mara

Kiongozi wa jumuiya ya Zimbabwe nchini Afrika Kusini Ngqabutho Nicholas Mabhena ana matumaini kwamba wenye ZEP wataweza kuhalalisha kukaa kwao Afrika Kusini, kutokana na muda ulioongezwa.

"Ongezeko hili ni suluhu kwa maelfu ya wamiliki wa vibali ambao wamekuwa wakihangaika kukamilisha makaratasi yao kulingana na agizo la Novemba 25, 2021 la baraza la mawaziri la Afrika Kusini," anaiambia TRT Afrika.

Kampuni ya huduma za usindikaji wa viza ya VFS imejukumiwa kufungua kituo cha Midrand au kituo kingine chochote kilichotengwa na ZEP ili kupunguza foleni.

"Tumewataka watoe thamani ya ada inayolipwa na waombaji. Pia tumetaka kuongeza uwezo wa tovuti yao na kuzingatia makosa ya mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na muda mdogo wa kujaza maelezo, pamoja na makosa mengine ya kiufundi. Tunatarajia mazungumzo haya yanazaa matunda na kusaidia kuharakisha maombi," anasema Mabhena.

Mwenyekiti wa kongamano la wahamiaji wa Zimbabwe, wakili Gabriel Shumba, anasalia kuwa na matumaini kwamba afueni inaweza kuja kupitia mahakama, ingawa uamuzi tayari umechukuliwa na idara na baraza la mawaziri katika ngazi ya kisiasa.

"Tunawaomba wamiliki wa ZEP kuhamia kwa visa za kawaida licha ya vikwazo," anasema.

Kabla ya kuongezwa muda, serikali ya Zimbabwe ilikuwa imejitolea kuwasaidia wale wote ambao walitaka kurejea nyumbani baada ya muda wa vibali vyao kumalizika. Takriban wahamiaji 8,000 wa Zimbabwe walikuwa tayari wamejiandikisha kuwa sehemu ya kundi la kwanza la waliorejea.

Michango ya kiuchumi

Raia wa Zimbabwe wanaochagua kurejea wamepewa njia maalum na Mamlaka ya Mapato ya Zimbabwe kusafirisha mali zote zinazomilikiwa kikamilifu kabla ya tarehe ya kuwasili nchini humo bila ushuru.

Kuna maelfu ya wahamiaji wa Zimabbwe nchini Afrika Kusini Picha : Reuters

Dola ya Zimbabwe inazidi kupanda, na kulazimisha wauzaji reja reja kuhangaika kutafuta majibu kwa bei kuongezeka maradufu ikilinganishwa na wiki zilizopita, na kusababishia kero mpya utawala wa Rais Emmerson Mnangagwa kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Kile kilichojulikana kama kikapu cha mkate cha Afrika kilipatwa na hali isiyotarajiwa mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Mgogoro nchini humo tangu wakati huo umekuwa na matokeo mabaya kwa eneo hilo kwa ujumla kwani Zimbabwe iko katikati mwa kusini mwa Afrika, kulingana na Rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chissano.

Alitoa maoni haya wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mazungumzo ulioandaliwa kuhusu malimbikizo na utatuzi wa deni. Ukuaji wa uchumi kwa ujumla umekuwa tete katika muongo mmoja uliopita, ukiashiriwa na mfumuko wa bei wa juu, viwango ada tofauti za ubadilishaji wa sarafu, na viwango vya madeni wasiyoweza kumudu.

Yote haya kwa pamoja yameongeza gharama ya uzalishaji na kupunguza motisha kwa uwekezaji unaoongeza tija.

Raia wa Zimbawbe wanaoishi Afrika Kusini na Uingereza walichangia kiasi kikubwa cha fedha zilizotumwa mwaka jana, na kufikia dola bilioni 1.66 kutoka dola bilioni 1.43 mwaka 2021, data rasmi inaonyesha.

Mvutano unaotishia

"Tunaona baadhi ya masuala yakichochewa na vuguvugu la chuki dhidi ya wageni kwa ajili ya uchumi unaotoka katika janga la Covid-19 - uchumi ambao unakabiliwa na changamoto kama vile umeme," anasema Gibson Nyikadzino, mchambuzi wa kisiasa. kuotka Harare, Zimbabwe.

Zimbabwe wanaishi Afrika Kusini wamehangaika kwa miaka mingi bila kujua hatma yao Picha : Reuters 

Gorden Dzikiti, raia wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini, ana maoni kwamba muda uliotolewa kwa watu kutoka nchi yake kuhalalisha kukaa kwao ni mdogo sana.

"Haitoshi kabisa kuhudumia kila mtu, na pia haitoshi kwa watu kupata msamaha. Kwa hali yoyote, baada ya kupata msamaha, unahitaji kuomba kibali cha jumla cha kazi. baada ya kupeleka ombi kwa wizara ya mambo ya ndani, itachukua miezi nane au zaidi kupata majibu," anaeleza.

Wakili Simba Chitando, ambaye anawakilisha Chama cha Wenye Vibali vya Zimbabwe katika vita vya kisheria na wizara ya mambo ya ndani katika Mahakama Kuu ya Pretoria, anasema nyongeza hiyo inatoa afueni ya muda kwa wenye vibali.

"Chaguo pekee la kweli ni ukazi wa kudumu," anasema. Benki tayari zimeanza kutuma jumbe zikisema kwamba akaunti za wamiliki wa ZEP zitakwisha tarehe 31 Desemba 2023 - na hivyo kuzua hofu ya kuendelea kwa utata.

TRT Afrika